CAIRO, Misri
KLABU ya Zamalek imethibitisha mshambuliaji wao nyota, Mostafa Mohamed, yuko katika hatua nzuri za kujiunga na miamba ya jiji la Istanbul, Galatasaray kwa mkopo.
Nyota huyo amekuwa akihusishwa na kuondoka huku timu kadhaa za Ulaya zikionesha nia ya kutaka kumsajili mshambuliaji huyo ambaye pia anakipiga na kikosi cha taifa cha Misri.

Mchezaji huyo wa miaka 23 alikaribia kujiunga na Saint-Étienne inayoshiriki Ligi ya Ufaransa, lakini, kuvunjika kwa mazungumzo baina ya viongozi wa pande hizo mbili, kulifanya dili hilo kuingia gizani.

Galatasaray ilitumia nafasi hiyo kwa kuanzisha mazungumzo na viongozi wa Zamalek na anatarajiwa kutua Uturuki mwishoni mwa wiki hii kukamilisha taratibu za uhamisho wake.
Hata hivyo, atajiunga na Galatasaray kwa mkopo wa mwaka mmoja na nusu, lakini.

Atakua na nafasi ya kusajiliwa moja kwa moja endapo ataonesha kiwango cha kuridhisha.
Ada ya usajili wa mkopo kwa mshambuliaji huyo inatajwa kufikia dola za Marekani milioni mbili na ikiwa wataamua kumsajili moja kwa moja.
Anaweza kuchukua nafasi ya Mbaye Diagne wa Senegal ambaye atahamia West Brom kwa mkopo.(AFP)