NA ABOUD MAHMOUD

MABINGWA watetezi wa kombe la mapinduzi timu ya Mtibwa Sugar imeanza vyema kampeni za kutwaa taji hilo, baada ya kuifunga Chipukizi bao 1-0.

Mchezo huo ulichezwa kwenye dimba la Amaan majira ya saa 10:00 jioni ambao ulihudhuriwa na mashabiki kiasi, na pambano hilo lilikuwa kali kwa muda wote, ambapo licha ya kushinda Mtibwa walipata upinzani mkali kutoka kwa Chipukizi

Timu hizo zilikianza kipindi cha kwanza kwa kushambuliana kwa zamu kila mmoja akisaka bao la kuongoza, lakini hadi kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu iliyoweza kuona lango la mwezake.

Kuanza kipindi cha pili Mtibwa walianza kulishambulia lango la mwezake huku ikifanya mabadiliko ya kumtoa Salum Kanoni na kumuingiza  Ibrahim Hilika dakika ya 54.

Mabadiliko hayo yalileta neema kwa Mtibwa ambapo dakika ya 57 Mtibwa ilijipatia bao hilo pekee lililotiwa kimiani  na Ibrahim Hilika.

Katika dakika ya 60  Chipukizi nayo ilifanya mabadiliko kwa kumtoa mchezaji Ali Khamis  na kumuingiza Mundhir  Iman, ili kuongeza kasi ya mashambulizi kwa kutafuta bao la kusawazisha lakini walishindwa kutumia nafasi walizozipata.

Michuano hiyo itaendelea leo kwa kupigwa mchezo mmoja katika dimba la Amaan, kwa kuzikutanisha timu za Mlandege na Malindi majira ya saa 2:15 usiku.

Mgeni rasmi katika mechi hiyo alikuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita  .