ZANZIBAR kama zilivyo nchi nyengine barani Afrika, ilijipatia uhuru wake kwa njia ya mapinduzi yaliyofanyika tarehe kama ya leo miaka 57 iliyopita yaliyoongozwa na Rais wa Kwanza, mzee Abeid Amani Karume.

Kufanikiwa kuratibu na kuyatekeleza mapinduzi hayo ndiko kulikofanikisha kuangushwa kwa utawala kisultani ambao uliiongoza Zanzibar chini ya miongozo na maelekezo ya waingereza.

Fahari ya kipekee katika mwaka huu wa 57 wa mapinduzi ni kwamba yanasherekewa kukiwa na awamu mpya ya uongozi wa awamu ya nane, chini ya rais kijana jasiri na mpambanaji huyu ni Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Kwa maono yake Dk. Mwinyi, shamrashamra na kilele cha sherehe za mwaka huu zisherekewe kwa namna ambayo haijapata kushuhudiwa na ambayo ni shirikishi zaidi kwa wananchi wote na isiyotumia gharama kubwa.

Mapinduzi yalikuwa na malengo mengi ambapo mbali ya kuwapatia uhuru, heshima, kurejesha utu wa wananchi, pia yamewafanya wazanzibari kuwa na uwezo wa kujiamulia mambo yao na kujipangia mustakbali wa maisha yao.

Mapinduzi pia yalilenga kuhakikisha yanastawisha maisha ya wananchi wanyonge kwa kuhakikisha wanapata huduma za muhimu za kimaisha ikiwemo elimu, afya, maji safi, makaazi na kadhalika.

Tunadiriki kusema kwa fahari kubwa kwamba katika kipindi cha miaka 57 ya mapinduzi ya Zanzibar, hakuna mwananchi anayeishi Zanzibar ambaye hajanufaika kwa namna yoyote ile na matunda ya mapinduzi.

Kwa wale wanaoyabeza na kuyadhihaki kwa sababu tunajua wapo, hata uhuru wanaoutumia wa kutoa kauli zao chafu dhidi ya mapinduzi, uhuru huo umeletwa na mapinduzi kwa sababu Zanzibar chini ya ukoloni wananchi hawakuwa na fursa ya kutoa maoni yao.

Kwa sasa tunadhani wakati umefika tuyaelekeze mapinduzi kwenye upande wa kiuchumi, tunajua hili limefanywa na awamu zilizopita, hata hivyo katika awamu iliyopo hii iwe ajenda yetu nambari moja.

Hakuna wakati muhimu zaidi wa kuelekea kwenye mapinduzi ya kiuchumi kama wakati huu, kwani tukifanya hivyo kwa hakika serikali yetu itakuwa imefanikiwa kuzitimiza ndoto za wananchi wake.

Ukweli ni kwamba Zanzibar inahitaji miradi mikubwa ya uwekezaji ikiwemo viwanda vitakavyotoa tija na kupunguza changamoto ya ajira, wazanzibari wanahitaji kunufaika na rasilimiali za asili kama gesi, mafuta, bahari nakadhalika.

Inaonekana tumechelewa kuangalia upande huu wa mapinduzi na badala yake tulizama sana kutoa simulizi za mapinduzi, hivyo tuiunge mkono kuali ya Dk. Mwinyi kwamba umefika wakati kwamba wananchi wanataka matunda ya mapinduzi na sio simulizi za mapinduzi.

Lakini huku tukikusanya nguvu za pamoja kuingia kwenye mapinduzi ya kiuchumi, serikali ya awamu ya nane lazima ihakikishe ina viendeleza vita ilivyovianzisha vya kupamabana na wahujumu uchumi, wazembe, wasioajibika, wezi na mafisadi.

Bila ya kuwadhibiti watu wa aina hii, itakuwa sawa na kuchota maji kwa pakacha, linapozama kisimani limejaa linapofika juu hamna maji. Kwa maana ya kwamba wengine wanatumia nguvu na jasho kujaza pakacha wengine wanajinufaisha.

Mapinduzi daima.