KIGALI, Rwanda
WAZIRI wa Michezo wa Rwanda, Aurore Mimosa Munyangaju, amewaambia wachezaji wa timu ya taifa ya soka wanaokwenda kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika (CHAN), kwamba Wanyarwanda wana matarajio mengi kutoka kwao, na wanapaswa kufanya kazi kwa bidii kuinua juu bendera ya taifa kwenye mashindano hayo.


Munyangaju alisema hayo wakati alipofanya ziara kwenye kambi ya timu hiyo itakayopeperusha bendera nchini Cameroun ambako mashindano hayo yatafanyika.
Kuanzia Januari 16, michuano hiyo itakusanya timu 16 kutoka bara lote ikiwemo Rwanda.
Ushindani huo ni wa kipekee kwa wachezaji ambao hushiriki kwenye ligi za ndani za nchi zao.


Amavubi waliondoka kwenda jiji la Doula, Cameroun juzi ikiwa na wachezaji 30 na wafanyakazi 21, ambao wote wamepimwa virusi vya ‘corona’.
“Kwa siku kadhaa, kumekuwa kukisika kile Wanyarwanda wanatarajia kutoka kwenu, ushindi na kiburi cha taifa. Hii inamaanisha kuwa bado wana imani na nyinyi kufanikisha hili, na mna uwezo wa kufanya vizuri, ”Munyangaju aliwaambia wachezaji na wafanyakazi wa Amavubi.


Hii itakuwa mara ya nne ambapo Rwanda itakuwa ikishiriki katika mashindano ya CHAN tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mnamo 2009.
Katika mechi zake tatu zilizopita, nchi hiyo imepata mara moja tu kupita hatua ya makundi na hii ilirudi mnamo 2016 wakati nchi ilipokuwa ikiandaa mashindano hayo.


Michezo ya mwaka huu itaandaliwa miji ya Yaounde, Douala, na Limbe nchini Cameroun.
Rwanda ipo katika kundi ‘C’ pamoja na nchi jirani za Uganda, Morocco na Togo.(Goal).