SIKU chache zilizopita ilimwengu uliuaga mwaka 2020 uliokuwa na chingu ya mambo na vijambo na kuukaribisha mwaka mpya wa 2021, ambao nao bila shaka utakuwa na matukio mengi.

Hata mwaka 2020 kwenye tasnia muhimu ya uandishi wa habari duniani ulikuwa mbaya sana kwani kulishuhudiwa waandishi wengi wa habari wakiuawa na wengine kukumbana na vizingiti katika kutekeleza majukumu yao.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na taasisi ya waandishi wa habari wasiona mipaka duniani (Reporters Without Borders), inakisiwa kwamba kiasi cha waandishi wa habari wapatao 50 walipoteza maisha wakiwa kwenye kazi zao ndani ya kipindi cha mwaka 2020.

Kwenye mazungumzo mafupi mkuu wa kamati ya usalama wa waandishi wa habari nchini Afghanistan, Najib Sharifi, alisema kwamba nchi hiyo haijawahi kuwa ya kuogofya kama ilivyo sasa.

Alisema mazingita ya kazi kwa waandishi wa habari yamekuwa magumu sana kiasi cha kufikia hatua ya kila muandishi wa habari yuko hatarini kupoteza maisha.

Ndani ya kipindi cha wiki sita nchini Afghanistan ilipoteza waandishi wanne wa habari na wote ama waliuawa kwa risasi au kwa mabomu yaliyotegeshwa kwenye gari zao.

Hali ni hivyo hivyo kwenye maeneo mengine ya ulimwengu, kwa mujibu wa Shirika la Waandishi wa Habari Wasiokuwa na Mipaka (RSF), katika ripoti yake hiyo ya pili kutolewa.

Ingawa idadi ya waandishi wanaouawa wakiwa wanaripoti matukio ya mapigano imepungua, wale wanaouawa kwa kudhamiriwa imeongezeka maradufu.

Waandishi wa habari 40 kati 50 waliouawa mwaka katika mwaka 2020 uliomalizika hivi karibuni, wamekufa kwa kulengwa kwa makusudi na watu wenye silaha.

Mtangazaji wa kituo cha televisheni nchini Afghanistan, Malala Maiwand, aliuawa mapema mwezi wa Disemba mwaka jana, katika mashambulizi ambayo kundi lijiitalo dol la kiislamu lilidai kuhusika.

Lakini Sharifi alisema kwamba si rahisi kuwatambuwa wahusika na malengo yao, hasa ikizingatiwa kuwa zamani Taliban na kundi hilo la dola la kiislamu walikuwa wakibebeshwa tuhuma za mauaji kama hayo, lakini sasa tangu Taliban na serikali ya Afghanistan kuanza mazungumzo ya amani ni vigumu kumtambua muhusika.

Ripoti hiyo inaonesha kwamba kwa mara nyengine tena nchi ya Mexico imeshika nafasi ya juu miongoni mwa mataifa yaliyo hatari sana kwa waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo waandishi wanane waliuawa mwaka 2020 wakati wakichunguza vitendo na matukio ya uhalifu wa kupanga na ufisadi.

Nchini Iraq ilipoteza waandishi watatu wa habari ambao walikuwa wakiripoti maandamano ya umma dhidi ya serikali mwezi Januari mwaka 2020, ambapo mmoja kati yao alilengwa kwa makusudi na watu wenye silaha ambao walitaka kuvizuia vyombo vya habari visiripoti maandamano hayo.

Nchini Pakistan, muandishi wa habari, Zulfiqar Mandrani alikutikana ameshakufa mwezi Mei mwaka 2020, huku mwili wake ukiwa na alama mwilini za kupewa mateso makali.

Marafiki na wenzake kazini wanadai kuwa kifo chake kilitokana na uchunguzi aliokuwa akifanya juu ya kesi ya dawa za kulevya ambayo inahusisha maovu yaliyotendwa na maofisa wa jeshi la polisi nchini humo.

India nayo imewekwa kwenye orodha ya mataifa matano yaliyo hatari kabisa kwa waandishi wa habari duniani, kutokana na waandishi wa habari katika taifa hilo kuwa kwenye mazingira magumu kutekeleza majukumu yao.

Tangu mwaka 2010, shirika hilo la kutetea waandishi wa habari, limesajili vifo vya waandishi watano wa habari nchini India kila mwaka, ambapo kwa mwaka 2020, shirika hilo limesajili vifo vine.

Taarifa zinaeleza kuwa vifo vya waandishi hao wa India vinahusishwa kufanywa na magenge ya uhalifu ambayo hapandi kuripotiwa kwa vitendo wanavyovifanya.

Ugunduzi huo umethibitishwa na kamati ya kuwalinda waandishi wa habari ulimwenguni (CPJ), ambayo inasema waandishi wa habari wa India wanakabiliwa na vitisho na mashambulizi kutoka makundi ya wahalifu na pia maofisa wa serikali.

Katika ripoti yake CPJ ilitaka uchunguzi wa kina wa mauaji ya mwandishi wa habari Rakesh Singh, aliyeuawa kwa bomu mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka 2020.

Mapema mwezi Disemba mwaka 2020, Iran ilimnyonga mwandishi wa habari mwenye maskani yake nchini Ufaransa, Ruhollah Zam, akiwa wa kwanza kunyongwa ndani ya kipindi cha miaka 30.

Mwandishi huyo alipewa adhabu hiyo kwa tuhuma za kuchochea maandamano dhidi ya serikali mwaka 2017 kupitia chaneli yake ya ujumbe mfupi kwenye mtandao wa Telegram. Ruhollah alitekwa akiwa ziarani Iraq na akafungwa jela nchini Iran.

Shirika la Waandishi wa Habari Wasiokuwa na Mipaka pia limesema kwamba kuna mamia ya waandishi wa habari waliopoteza maisha yao mwaka 2020 kutokana na maradhi ya COVID-19.

Baadhi ya vifo hivyo vilihusiana na kazi zao za kuripoti, ambapo watatu kati yao vikiwa katika mataifa ya Urusi, Misri na Saudi Arabia, ambako waandishi wa habari walikamatwa wakiwa kwenye kazi zao na kisha wakafa kwa COVID-19 kutokana na kunyimwa ruhusa ya kupatiwa matibabu.