NA MARYAM HASSAN

MWANADADA wa miaka 20, amepandishwa katika kizimba cha Mahakama ya mkoa Vuga kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya.

Nasra Moris Raphael mkaazi wa Fuoni Melitano, amepanda kizimbani hapo mbele ya Hakimu Hussein Makame na kusomewa shitaka lake na wakili wa serikali, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Fatma Saleh.

Akiwa mahakamani hapo, wakili huyo alidai mshitakiwa huyo apatikana na dawa za kulevya, kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha sheria nambari 9 ya mwaka 2009.

Wakili huyo alisema, mshitakiwa alitenda tukio hilo Disemba 28 mwaka jana majira ya saa 1:00 za usiku huko Fuoni Melitano wilaya ya Magharibi’B’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa bila ya halali, alipatikana na kifuko cha plastiki chenye kuonesha, ndani yake mkiwa na vijiwe 12 rangj ya brouni ambavyo zinasadikiwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroini.

Alisema vijiwe hivyo vilikuwa na uzito wa gramu 2.975 kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mara baada ya kusomewa shitaka lake mshitakiwa huyo alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana.

Ombi la mshitakiwa huyo limepingwa kwa sababu Kiwango alichopatikana nacho ni kikubwa.

Aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo na kupangwa tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi.

Maelezo hayo aliyatoa mbele ya Hakimu Hussein Makame, ambapo alikubaliana na ombi la wakili huyo.

Hakimu aliamuru mshitakiwa kupelekwa rumande hadi Januari 20 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi.