Mahakama maalum mbioni kuundwa

NA KHAMISUU ABDALLAH

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema umefika wakati sasa kwa Zanzibar kuanzisha mahakama maalum itakayokabiliana na makosa ya udhalilishaji ili kupunguza mrundikano na ucheleweshaji wa kesi za uhalifu huo.

Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mkutano wa wadau wanaohusika na masuala ya udhalilishaji katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil uliopo Kikwajuni.

Alisema tayari ameshazungumza na Jaji Mkuu na kukubaliana kimsingi kuanzishwa mahakama hiyo ambayo itatoa fursa ya kushughulikia kesi hizo na kufikia lengo la kuondoa malalamiko kwa wananchi.

Alifahamisha kuwa katika kulifanikisha hilo watendaji wa taasisi zote zinazohusika na masuala ya kisheria wanapaswa kujitathmini juu ya utendaji wao na kufanya mabadiliko ya sheria kwa haraka ili kuweka sheria zitakazokidhi mahitaji.

Dk. Mwinyi alisema tatizo la udhalilishaji ni kubwa na linaleta aibu katika nchi na maumivu makubwa kwa wananchi walio wengi na lisipokemewa litaendelea kuharibu watoto.

Alisema lipo tatizo la msingi linalohitaji ufumbuzi kwa kushirikiana pamoja ikiwemo serikali, wananchi, mahakama, Ofisi ya DPP, Jeshi la Polisi ikiwemo utoaji wa elimu kwa jamii ili kukinga tatizo hilo kabla halijatokea.

Aidha alisema anatambua wapo wanaharakati, viongozi wa dini, masheha, waratibu na taasisi zisizo za kiserikali wanafanya kazi katika jamii, lakini tatizo linaendelea kuwepo hivyo imefika wakati kuchukuliwa hatua kali dhidi yao.

Hata hivyo, alisema bado taasisi zote zina jukumu la kurekebisha kasoro zao ikiwemo polisi kuacha kupatanisha kesi hizo baina ya mkosaji na aliyekosewa kifamilia.

Dk. Mwinyi alizitaka taasisi zote ikiwemo mahakama, polisi na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kujipanga upya katika kukabiliana na tatizo hilo ili lisiendelee kupoteza nguvu kazi ya taifa.

Alibainisha kuwa bado kazi ya ziada inahitajika katika mahakama kwa kuhakikisha wanapunguza muda wa kufuatilia kesi hali ambayo inapelekea wananchi kukata tamaa kufuatilia kesi zao.

Hata hivyo, alisema wakati umefika kufumua sheria ambazo zinakuwa kikwazo katika masuala hayo kwa kuja na sheria muafaka katika kukomesha vitendo hivyo.

Dk. Mwinyi aliwaagiza wale wote wanaoshughulika na masuala ya sheria serikalini kukaa chini na kulifanya jambo hilo kwa haraka ili Baraza litakalokaa mwezi wa Februari mwaka huu liende na mabadiliko ya sheria hizo.

Sambamba na hayo, alisema sheria inahitaji wadau wengi hivyo aliwaomba wadau na vyombo vyote vinavyohusika na masuala hayo kushirikiana na serikali ili kufanya marekebisho ya sheria hizo na kuondoa mkwamo katika kushughulikia masuala ya udhalilishaji.

Dk. Mwinyi aliwasisitiza wanahabari kuwa na jukumu la kutoa elimu kwa jamii kwa kuandaa vipindi vya vinavyohusiana na udhalilishaji ili wananchi kutambua mambo mbali mbali ikiwemo kuuhifadhi ushahidi kama kielelezo katika kesi na kutocheleweshwa kupelekwa mhanga katika sehemu husika.

Mbali na hayo, alisema ni vyema kwa Wizara ya Afya kutengeneza mkakati wa kuimarisha maeneo maalum ya upimaji wa waathirika katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuondoa usumbufu kwa wahanga.

Akizungumzia skuli na madrasa, alisema wakati umefika kuangalia mitaala ya elimu ili kutoa nafasi kwa wanaharakati kupewa nafasi kuzungumza na watoto na walimu kupewa elimu ya kuzungumza na wanafunzi katika kuwakinga na matukio hayo.

Alisema walimu wa madrasa ndio wanaoshutumiwa hivyo ni vyema kwa taasisi za dini kujiangalia kwa kufanya tathimini katika taasisi zao na kuzuia walimu wanaotuhumiwa kwa mambo hayo kusimamishwa mara moja.

Akizungumzia suala la rushwa na urasimu alisema tatizo hilo lipo katika maeneo yote na wasipolisema basi halitaweza kutatuliwa na kuzitaka mahakama, polisi na hospitali kujitathmini katika kufanya kazi zao kwa kuzuia rushwa katika taasisi zao.  

Hivyo alisisitiza Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) kuongeza bidii katika kupambana na rushwa katika maeneo yote na kutafuta njia ya kuondoa urasimu katika kushughulikia mambo hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashitaka kutoka Ofisi ya DPP, Ibrahim Mzee, alisema mwaka 2020 kesi walizopokea zilikuwa ni 531 na mikoa inayoongoza ilikuwa ni Mjini kwa kesi 248, Kaskazini kesi 58, Kusini kesi 80, Kaskazini Pemba kesi 64, Kusini Pemba kesi 81 huku kesi walizopeleka mahakamani zilikuwa 404 mafaili 110 walitoa maamuzi yaendelee na upelelezi na mafaili 43 yalikuwa hayana ushahidi.

Aidha alisema kesi 414 zilifunguliwa mahakamani ikiwemo wilaya, Mkoa na mahakama ya watoto, kesi 62 zilitiwa hatiani, walioachiwa huru 43 zilizoondoshwa 51 na kesi zilizoondoshwa na upande wa mashitaka zilikuwa kesi saba. 

Aidha alibainisha kuwa changamoto ya kisheria inasababisha kuongezeka kwa makosa ya udhalilishaji nchini.

Amina Yussuf Ramadhan ni mwanaharakati wa kupinga masuala ya udhalilishaji alisema yapo makundi yanayosababisha kuunga mkono masuala hayo kwa kutaka suluhisho katika ngazi za kifamilia.

Akizungumzia vichocheo vinavyosababisha kuongezeka kwa matukio hayo alisema ni wingi wa baa katika makaazi ya watu, mmong’onyoko wa maadili, vituo vya polisi kuwa gesti bubu na utalii usiozingatia maadili ya kizanzibari.

Akizungumzia mafanikio waliyoyapata alisema ni pamoja na jamii kupata muamko juu ya kuripoti matukio hayo na kudai haki zao pale wanapokosa na kuweza kusaidia wahanga 200 kurekebisha tabia zao.

Nao washiriki wa mkutano huo walisema imefika wakati kuwa na uwazi katika kusimamia matukio hayo kwa kuweka mikakati maalum ili kuondoa vitendo hivyo.

Mzuri Issa kutoka Tamwa Zanzibar alisema sheria ina mapungufu mengi ikiwemo sheria ya ushahidi ambazo zimekuwa zikikinzana kwa kiasi kikubwa.

Naye Jamila Mahmoud kutoka ZAFELA alisema rushwa inachukua nafasi kubwa katika kutoa haki katika vitendo vya udhalilishaji hivyo alishauri kushirikiana pamoja kila mmoja kwa nafasi yake katika kuliondoa tatizo hilo.