NA MWAJUMA JUMA

KAMPUNI ya Ubebaji mizigo Zanzibar katika uwanja wa ndege (ZAT), imekabidhi zawadi za washindi wa michuano ya  kombe la Mapinduzi yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 5 mwaka huu.

Makabidhiano ya zawadi hizo yalifanyika jana katika ukumbi wa mkutano wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, ambapo Mwenyekiti wa Kampuni hiyo Mohammed Raza alimkabidhi waziri wa wizara hiyo Tabia Maulid Mwita.

Zawadi zilizokabidhiwa ni kombe kubwa la mshindi wa kwanza kwa timu za wanaume na wanawake washindi wa pili na watatu kwa timu zote.

Zawadi nyengine ni medali pamoja na zawadi ndogo ndogo kwa ajili ya wachezaji bora wa mashindano kwa upande wa wanaume.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi zawadi hizo Raza aliitaka kamati inayosimamia mashindano hayo kufanya kazi kwa kujitolea ili kwenda sambamba na malengo ya kuanzishwa kwa mashindano hayo.

Alisema mashindano hayo yameanzishwa yakiwa na lengo la sherehe lakini pia kwa ajili ya kukuza vipaji vya wanamichezo wao.

“Haya mashindano ni ya kujitolea tunatakiwa tuyasimamie kwa nguvu zetu ili yaweze kwenda kama yalivyopangwa”, alisema.

Kwa upande wake waziri Tabia alitoa wito kwa wadau wengine kujitolea kusaidia kutoa michango yao kwa hali na mali ili kuunga mkono juhudi za rais wa Zanzibar katika kuendeleza michezo.

Alisema kila mmoja anapaswa kuunga mkono juhudi za kuinuwa michezo katika visiwa hivi ili vijana wao waweze kufaidika nayo.

“Tunakuwa tunafarijika sana kuona wadau wanajitokeza kusaidia michezo, hivyo kuna haja na watu wengine kujitolea ili kufanikisha mashindano yetu”, alisema.

Michuano ya kombe la Mapinduzi yanashirikisha timu tisa zikiwemo nne za Zanzibar na tano za Tanzania Bara yatakuwa yakichezwa katika uwanja wa Amaan .

Timu hizo zinazoshiriki ni Mtibwa Sugar, Simba, Yanga, Azam FC, Namungo FC, Jamhuri, Chipukizi, Malindi na Mlandege.