TIMU ya soka ya New Generation imefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya mapinduzi kwa soka la Wanawake kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Jumbi.


Mchezo huo wa fainali ulichezwa jana kwenye uwanja wa Mao Zedong saa 10:00 za jioni na kutoa ushindani wa hali ya juu.


Katika fainali hiyo kila timu zilishuka uwanjani hapo ikiwa na ari moja ya kutaka kushinda mchezo huo ambao ulihudhuriwa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Lela Mussa ambae alikuwa mgeni rasmi.


Wakicheza kwa kushambuliana kwa zamu na kufanikiwa kwenda mapumziko kwa timu ya New Generation ikiongoza kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mwajuma Abdalla dakika ya 11 na Warda Abdulhakim dakika ya 29.


Kipindi cha pili kilianza na miamba hiyo kuendelea kushambuliana, ambapo New Generation wakaongeza bao la tatu lililofungwa tena na Mwajuma Abdalla dakika ya 76 kwa mkwaju wa penalti.


Katika mashindano hayo pia kulitolewa zawadi ya mchezaji bora Neema Suleiman wa Jumbi pamoja na mfungaji bora Mwajuma Abdalla aliyefunga mabao 12 na kuondoka na kiatu cha dhahabu.

Bingwa wa michuano hiyo ambayo ilishirikisha timu tisa alipata kombe na medali za dhahabu wakati mshindi wa pili aliondoka na kikombe na medali za fedha.


Aidha katika michuano hiyo mapema kulifanyika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu uliowakutanisha New Sister na Feuture Queens, ambapo timu ya New Sister ilitwaa nafasi hiyo kwa ushindi wa mabao 2-0 na kukabidhiwa zawadi ya kikombe.