NA MWAJUMA JUMA

TIMU za Soka za Simba, Namungo na Yanga zimefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya kombe la mapinduzi yanayoendelea visiwani Zanzibar.

Namungo imefanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kupata nafasi ya mshindwa bora (best Looser), wakati Simba na Yanga walifikia hatua hiyo baada ya kushinda katika michezo yao.

Simba ambayo ilikuwa katika kundi B imeshika nafasi ya kwanza baada ya kushinda michezo yote miwili na kuvuna pointi sita kundi ambalo lilikuwa na bingwa mtetezi timu ya Mtibwa ambayo imeutema ubingwa huo kwa kufungwa mabao 2-0.

Hivyo Simba kwa matokeo hayo itacheza na Namungo katika mchezo wao ambao utachezwa majira ya saa 2:00 usiku
katika uwanja wa Amaan.

Kwa upande wa timu ya Yanga wao watashuka dimbani leo pia anasubiri matokeo ya mchezo uliopigwa jana usiku baina ya Azam na Malindi.

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo nusu fainali hiyo ya Yanga ambao wameingia kwa kuwa na pointi nne kutoka kundi A, itachezwa majira ya saa 10:00 za jioni uwanjani hapo.