DOHA,  Qatar

MSHAMBULIAJI Michael Olunga aliamua kwenda  nchini Qatar kuchezea kikosi cha Al Duhai SC baada ya kuvunja mkataba na klabu ya Kashiwa Reysol ya Ligi Kuu ya Japan (J1 League).

Hatua hiyo ya Olunga inamfanya kuwa Mkenya wa pili baada ya nahodha wa zamani wa Harambee Stars, Dennis ‘The Menace’ Oliech kucheza soka ya kulipwa nchini Qatar.

 Taifa hilo liliwahi kumpa Oliech ofa ya mamilioni ya pesa ili abadilishe uraia wake na kupata ule wa Qatar.

Mbali na kuchezea Nantes, AJ Auxerre na AC Ajaccio za Ufarasa, Oliech aliwahi pia kuchezea Dubai CSC katika Falme za Kiarabu (UAE) kabla ya kutundika rasmi daluga zake akivalia jezi za Gor Mahia mnamo 2019.

Chini ya kocha Sabri Lamouchi ambaye ni raia wa Ufaransa, Al Duhail kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ya vikosi 12.