NA MADINA ISSA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, ameitaka mamlaka ya usimamizi wa shughuli za Bima Tanzania (TIRA), kuongeza taaluma ili jamii ihamasike kutumia bima.
Aliyasema hayo alipokuwa akifungua semina ya siku moja kwa wakuu wa mikoa, wilaya na masheha wa Unguja, inayohusiana na uelewa wa bima iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakili Kikwajuni Mjini Unguja.
Alisema kumekuwa na dhana mbaya kwa jamii kuhusiana na suala la bima hali inayotokana na uelewa mdogo kwa wananchi hao na kusababisha baadhi ya wananchi kutokata bima ya aina yoyote kwa kuhofia kutokuwa na manufaa nayo.
Alisema ni vyema mamlaka hiyo ikahakikisha mwananchi aliyekata bima anapatiwa stahiki zake kwa wakati endapo atakapopatwa na majanga kwa usimamizi wa hali ya juu.
Alisema kwa sasa mamlaka hiyo inapaswa kujitathmini juu ya hali ya ukataji bima hiyo ili kuona wanawafikia wananchi na kutambua umuhimu wake katika kuwalinda na majanga mbali mbali dhidi ya harakati zao ikiwemo biashara.
Aidha waziri huyo alizitaka taasisi zinazotoa huduma hizo kuimarisha huduma zao katika kwenda na wakati na kuondoa urasimu katika kuwahudumia wananchi.
Sambamba na hayo, alisema kuwa serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi, isingependa kuona wananchi wake wanarejeshwa nyuma kimaendeleo kutokana na athari mbalimbali zinazosababishwa na majanga mbalimbali.
Pamoja na hayo, aliwataka wananchi na wafanyabiashara kukatia bima mali zao ikiwemo biashara ili kuweza kuepuka hasara zinazotokana na majanga yasiyotarajiwa.
Mapema Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania, Khadija Issa Said, alisema, lengo la mamlaka hiyo ni kuona wanafikia asilimia 80 ya wananchi kuwa na uelewa juu ya masuala ya bima zikiwemo za maisha, Elimu na nyenginezo ifikapo mwaka 2025.
Alisema kuwa mamlaka imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika kuona elimu inawafikia wanajamii, ikiwemo, kutoa elimu kwa wananchi vijijini, matangazo mbalimbali na vipeperushi pamoja na matamasha mbalimbali yanayokuwepo nchini.
Sambamba na hayo, alisema kuwa kwa sasa soko la bima limekuwa na zaidi ya makampuni 10 kati ya makampuni 32 yaliyosajiliwa na Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania ambayo yalifungua makampuni yake Zanzibar.