NA ASYA HASSAN

TAASISI ya Panje Project ina mpango wa kufanya maonyesho ya kazi za uchoraji kwa wachoraji wa ndani na kubadilishana na wachoraji wengine wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na Zanzibarleo, Mwalimu wa somo la sanaa ya uchoraji katika taasisi hiyo, Masoud Muhidin Masoud, alisema hatua hiyo itasaidia kuzitangaza bidhaa hizo pamoja na kupata masoko ya uhakika.

Alisema taasisi hiyo imekuwa ikitoa taaluma hiyo kwa vijana wa maeneo ya Nungwi ili wajiajiri wenyewe na kuondokana na tatizo la ajira.

Alifahamisha kwamba vijana hao wanapatiwa elimu hiyo na mbinu nyengine ili waweze kujiajiri wenyewe kwani kufanya hivyo kutafanikisha lengo la taasisi hiyo kuwapatia taaluma vijana nchini.

Alifahamisha kwamba kijiji cha Nungwi, kimepiga hatua kubwa katika sekta ya utalii lakini asilimia kubwa ya vijana na wenyeji wa kijiji hicho wapo nje ya soko la ajira kupitia sekta hiyo kutokana na kutokuwa na elimu au ujuzi.

“Kutokana na kukua kwa sekta ya utalii katika kijiji hiki hasa uwepo wa hoteli pamoja na mikahawa mategemeo yetu itakuwa chachu ya vijana hawa kupata nafasi za ajira kutokana na ujuzi wanaopatiwa,” alisema.

Akizungumzia vifaa mwalimu huyo alisema wana vifaa vya kutosha hivyo ni vyema jamii kuwa tayari kupeleka watoto wao ili kupata ujuzi ambao utawasaidia kupata ajira na kuendesha maisha yao.

Taasisi ya Panje yenye makao makuu yake Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja iliasisiwa mwaka 2011 ikiwa na jukumu la kuhakikisha inasaidia jamii kuipatia elimu ambayo itawawezesha vijana kujielewa na kujipatia ajira kwenye soko la utalii.