WASHINGTON,MAREKANI

SPIKA wa Bunge la Wawakilishi la Marekani amewaandikia barua wanachama wa chama cha Democratic na kusisitiza kuwa ushindi wa rais mteule wa nchi hiyo utathibitishwa katika kikao cha Kongresi.

Nancy Pelosi aliwaandikia barua wanachama wenzake wa Democratic ndani ya Kongresi ya Marekani kwamba kikao hicho cha pamoja kilichopangwa leo kitakuwa cha aina yake.

Katika barua yake hiyo Pelosi aliandika katika miaka ya karibuni walipitia matatizo mengi lakini hawawezi kulinganisha kipindi chochote na kipindi cha utawala wa Rais wa sasa wa Marekani Donald Trump na mienendo yake ya kutoheshimu matakwa ya wananchi.

Spika wa Bunge la Wawakilishi la Marekani aliashiria uwezekano wa kupingwa kura za majimbo kadhaa katika kikao hicho cha tarehe sita mwezi huu na kueleza kuwa upo uwezekano kutangazwa matokeo ya mwisho kukachukua muda.

Wabunge wa chama cha Republican katika Kongresi ya Marekani walijiandaa kupinga matokeo ya uchaguzi na ushindi wa rais mteule wa nchi hiyo, Joe Biden, katika kikao cha kutangaza maoni kuhusu matokeo hayo ya uchaguzi.

Trump na  Makamu wake, Mike Pence, waliunga mkono uamuzi wa maseneta wa chama chao cha Republican baada ya kutishiwa na Warepublican wenzao.