HIVI karibuni viongozi wa ligi daraja la kwanza Pemba walikutana na rais wa Shirikisho la Soka Zanzibar ZFF na kujadili mambo mbali mbali huko Pemba.

Katika mkutano huo viongozi hao wameushauri uongozi wa Shirikisho la Soka Zanzibar ( ZFF), kujitathimini kama wanastahiki kuendelea kukaa madarakani au kujiuzulu wenyewe.

Viongozi hao bila ya kutafuna maneno walisema hivi sasa kumekuwa na migogoro mingi ndani ya ZFF, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linazorotesha ukuaji wa mpira wa miguu Zanzibar, hivyo ni vyema viongozi hao wakajitathimini au kuondoka madarakani kulinda heshima yao.

Walikwenda mbali zaidi ka kusema kuwa Zanzibar wapo watu wengi ambao wanauwezo wa kuongoza mpira, hivyo ni busara kabisa viongozi wa juu ya ZFF, kukaa pembeni ili kupata viongozi wapya kwa maslahi ya nchi kwa ujumla.

Waliongeza kusema matatizo mengi ambayo yanajitokeza katika ligi hasa Pemba yanasababishwa na ZFF, hivyo ni ukweli kuwa viongozi hao wameshindwa kuongoza.

Lakini katika madai yao wanasema yote hayo yanayotokea ni kwa sababu ya uongozi mbovu wa ZFF, kujimilikisha madaraka yote bila ya kujali mustakbali wa mpira wa Zanzibar.

Katika mkutano huo viongozi hao walieleza mambo mengi sana ambayo mengine hata hayastahiki kuandikwa, bora yabaki kuwa ni siri lakini imani yangu viongozi hao ZFF wameyasikia.

Katika hili ni dhahiri kuwa hiki ninachokiandika hapa hakitawafurahisha baadhi ya watu, lakini vyema watanisamehe, ila ukweli bora usemwe kwa maslahi ya wengi, hasa sisi watu wa michezo tukiamini kuwa mpira ni mali ya watu si wa mtu mmoja au kikundi fulani.

Kumbwa nichotaka kusema, waswahili wamesema ‘Muungwana akivuliwa nguo basi huchutama’, hakika wahenga hawakukosea hata kidogo, kwani kuchutama kwake kutaleta stara kuliko kuendelea kusimama.

Hivi ndivyo ilivyo kwa viongozi wa ZFF, ambapo hivi sasa ni dhahiri kuwa soka la Zanzibar bado linayumba na linahitaji viongozi wenye uwezo mkubwa sana wa kuongoza, sina maana kuwa waliokuwepo hawafai, lakini kama walivyosema viongozi wa Pemba kuwa ZFF ya sasa wanatakiwa kujitathimini wenyewe jee wanautendea haki mpira wa Zanzibar.

Lakini pia wanapashwa kujiuliza wameutendea nini mpira wa Zanzibar, kuna tofauti gani viongozi waliondoka madarakani na wao ambao wapo sasa, jee tumepiga hatua gani, yale malalamiko mengi ambayo yalikuwa yalilalamikiwa kwa uongozi uliopita wameyatatua likiwemo suala zima la madeni ya waamuzi, jee hivi sasa hawadai, hayo ni baadhi ya masuala ambayo viongozi wa ZFF wanatakiwa kuyajibu na kama wameshindwa basi wanapashwa kujitathimini juu ya uwepo wao madarakani.

Pia viongozi wa ZFF wanapaswa kujibu suala kwa nini hadi sasa ligi daraja la kwanza kanda ya Pemba haijachezwa, wakati Unguja inaendelea, jee Pemba wana ZFF yao ndio imeshindwa kuendesha ligi hiyo.

Katika kikao hicho cha Pemba kiongozi mmoja wa ZFF alijaribu kujibu hoja kwa kukiri kuwa kulikua na sitofahamu nyingi pamoja na baadhi ya miongozo kwa upande wa Pemba haikua vizuri.

Alifahamisha kuwa si tatizo wao kuondoka madarakani lakini hadi sasa hajaona sababu ya kuondoka, labda kwa sababu zake binafsi na wala hatojutia kuondoka.

Hoja hizi za ZFF hazinishawishi kuona ZFF ina lengo la kutatua changamoto iliyopo, kwani hoja na masuala ambayo nimeyataja hapo juu, yanahitaji majibu mazuri ili wale wanaohoji hayo waridhike.

Hivi sasa ni dhahiri kuwa hali ya mambo ndani ya ZFF si swari japo wenyewe wameamua kuficha hili, kumekuwa na mvutano mkubwa baina ya viongozi wa ZFF na bodi zake, ZFF na timu hasa timu za Pemba na ndio maana mpaka leo ligi daraja la kwanza Pemba bado haijachezwa.

Sina lengo la kutoa shutuma au lawama kwa ZFF, lakini kama nilivyotangulia kusema mwanzo kuwa bora tuseme ukweli ili viongozi wapate kuyafanyia kazi kwa maisha ya soka letu,kuliko kukaa kimya na wao viongozi wakadhani wanachokifanya ni sawa.

Kumalizia hili niiombe Serikali kuliingilia kati suala hili mapema kabla halijaleta mzozo mkubwa na ligi ikashindwa kuchezwa Pemba. Kwani kumbukumbu zinaonyesha kuwa ligi daraja la kwanza Pemba msimu uliopita haikumalizika kutokana migogo.

Niitahadharishe serikali kuwa kama itaendelea kuwaonea haya viongozi wa ZFF na kuwaacha wafanye wanavyotaka basi hali ya soka la Zanzibar itaendelea kudidimia kama ambavyo ipo hivi sasa.

Lakini kwa lugha laini kabisa na nyepesi niseme wazi kuwa tumbua tumbua inayofanywa na serikali katika taasisi nyingine, basi umefika wakati sasa ihamie ndani ya vyama vya michezo tena ikianzia ZFF.