NEW YORK,MAREKANI

MAKAMU wa rais wa Marekani Mike Pence amemwambia rasmi spika wa bunge Nancy Pelosi kwamba haamini kuwa hatua ya kutumia ibara ya 25 ya katiba ya nchi hiyo kumuondoa Trump madarakani ni kwa manufaa ya nchi au hata kuendana na katiba.

Ujumbe wa Pence ulitokea wakati baraza la wawakilishi lilikuwa likijadili pendekezo la kutumia ibara hiyo ya 25.

Hata hivyo inatarajiwa kuwa wabunge wataendelea na mchakato wa bunge kwa lengo la kumuondoa Trump au kuzima matarajio yake kuwania urais baadaye.

Awali katika tukio tofauti, Rais Trump alisema ibara hiyo haitokuwa na maana yoyote kwake.

Trump alisema pia kuwa wito wa kutaka aondolewe madarakani kwa njia ya mashitaka bungeni vilevile ni mbaya zaidi.

Kwingineko, majenerali wakuu wa jeshi nchini Marekani, walishutumu uvamizi uliofanywa na wafuasi wa Rais Trump dhidi ya majengo ya bunge wiki iliyopita.

Kwenye taarifa ya pamoja iliyosainiwa na wakuu wanane wa kijeshi wakiongozwa na mwenyekiti wao jenerali Mark Milley, tukio hilo lilikuwa shambulizi la moja kwa moja dhidi bunge la Marekani na dhidi ya mchakato wa kikatiba.