NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

WAZIRI Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amesema kuwa Afrika inazaidi ya aina 400 za mazao ya mboga mboga za asili, lakini yanayotumika kwa chakula na biashara ni machache sana jambo ambalo linahitaji kuandaliwa mkakati maalum ili iwe na faida kwa bara la afrika.

Pinda alisema hayo Jana wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa taasisi za kilimo hapa nchini na nje ya nchi, wadau, wafanyabiashara na watafiti wa mboga mboga nchini na nje, lengo ni kutaka kuboresha zaidi kilimo hicho ili kiwe zao la kibiashara na chakula kwa faida ya nchi na Afrika kwa ujumla mkutano huo umeandaliwa na kituo cha World vegetable Centre cha Jijini Arusha.

Alisema mboga mboga za asili katika Afrika ni urithi wa waafrika na mazao hayo lazima yatunzwe kuenziwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuyatunza pamoja na kutunza bioAnuni {biodiversity} isipotee kwani ni muhimu kwa afya na lishe.

Waziri Mkuu huyo Mstaafu alisema utafiti unaonyesha kwamba kutokana na kutofanyiwa utafiti wa kutosha na changamoto za mabadiliko ya tabia mimea ya mboga mboga, hasa ile ambayo hailimwi inazidi kupotea kwa kasi kubwa sana na upoteaji huo ni hasara si tu kwa bara la Afrika bali kwa dunia nzima hivyo jitihada za ziada zinahitajika na mkutano huu utoke na jibu la suruhisho hilo.

Alisema mazao ya mboga mboga ni muhimu sana kwenye afya na lishe na utafiti wa kitaalamu unaonyesha kuwa mboga za asili zina viwango vikubwa vya viini lishe ukilinganisha na mboga zingine kutoka Mataifa ya nje ya Bara la Afrika kwani watafiti na wataalamu wengine wameyaita mazao haya ‘’super foods’’ yaani vyakula vyenye viini lishe bora kabisa.

Pinda alisema kufuatana na takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa {FAO} kuna takribani watu milioni 821 wanaokabiliwa na matatizo ya utapiamlo yanayotokana na kula chakula kisichokuwa na viini  lishe bora {malnutrition} kwa kwa upande wa hapa nchini hali ni mbaya sana katika suala la utapiamlo kulingana na takwimu za utafiti wa hali ya lishe za mwaka 2018.

Alisema takwimu hizo za mwaka 2018 zinaonyesha kuwa Watoto {miaka 0-5} milioni 3 wamedumaa,Watoto {miaka 0-5} milioni 1.3 wana uzito pungufu,Watoto {miaka 0-5} milioni 5 wana  upungufu wa damu,Watoto {miaka 0-5}  milioni 3 wana upungufu wa vitamini A na asilimia 32 ya wanawake{miaka 14 – 49} wana tatizo la uzito uliozidi{overweight}.

Waziri Mkuu huyo Mstaafu, alisema serikali kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo imeamua kupitia ilani ya chama chake cha Chama Cha Mapinduzi{CCM} ya mwaka 2020 hadi 2025 wameweka uzito mkubwa kwa kuahidi kufanyia kazi changamoto hiyo na ikibidi kumaliza kama sio kupunguza tatizo hilo.

Naye Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Taasisi ya World Vegetable Centre,Dk. Gabriel Rugalema, alisema kuwa lengo la mkutano huo mbali ya kuhamashisha wakulima kulima mboga mboga hapa nchini pia ni kutaka zao hilo hapa nchini kuwa zao kuu la kibiashara ili liweze kuingizia nchi mapato.

Dk. Rugalema, alisema na kuiomba serikali tafiti zinazofanywa na wataalamu ziwe zinafanyiwa kazi ili zije na malengo yenye kuboresha zao hilo la mboga mboga hapa nchini kw amustakabali wan chi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Asasi ya kuendeleza kilimo cha mboga mboga,matunda na maua hapa nchini {TAHA}, Jackline Mkindi, amesema kuwa iwapo serikali itatilia mkazo kilimo cha mboga mboga hapa nchini huenda zao hilo likawa mkombozi wa mwanchi katika kumwingizia kipato.