PYINMANA,MYANMAR
TAKRIBAN Warohingya 100, waliosafirishwa kimagendo kutoka jimbo linalokumbwa na machafuko la Rakhine nchini Myanmar, wamekamatwa na polisi waliofanya msako eneo la Yangon.
Kisa hicho cha hivi karibuni cha ulanguzi wa wanadamu kilifichuliwa na polisi wa Yangon baada ya kufanya msako katika nyumba mbili katika mtaa wa Shwepyitha na kuwapata Warohingya 99.
Maofisa wa polisi walisema Warohingya hao walikuwa wakielekea Malaysia ikiwa ni sehemu ya mtandao wa usafirishaji wa wanadamu kinyume na sheria.
Masaibu ya Warohingya yaligonga vichwa vya habari za kimataifa mnamo mwaka 2017, baada ya operesheni ya kijeshi dhidi yao katika jimbo la Rakhine, magharibi mwa nchi yao na kusababisha takriban watu 750,000 kukimbilia Bangladesh.