NA SAIDA ISSA, DODOMA

JESHI la Polisi nchini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA ) na Taasisi nyengine za usimamizi wa Sheria, linatarajia kufanya oparesheni nchi nzima dhidi ya Wafanyabiashara ambao  wamekuwa wakikwepa kulipa kodi na wanaokaidi  kutumia mashine za kielektroniki EFD mashine.

Hatua hiyo inakuja kufuatia Jeshi hilo kubaini kuwepo kwa baadhi ya wafanyabisha nchini pamoja na Taasisi za biashara wanaokwepa kodi kwa kufunga Maduka madogo na wengine kufanya biashara zao kwenye maghala bila kulipa kodi jambo ambalo linarudisha nyuma uchumi wa nchi

Hayo yameelezwa  Jijini Dodoma na Kamishina wa Polisi, Utawala na menejimenti ya rasilimali watu CP, Benedict Wakulyamba, kwa niaba ya Inspekta wa Polisi Jenerali Simon Sirro, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na  oparesheni hiyo.

Kamishna huyo katika kikaoa hicho alitoa maagizo kwa makamanda wa polisi wote nchini Tanzania pamoja na Zanzibar,  kuhakikisha wanakabiliana na wafanyabiashara hao wanaokwepa kodi.

“Jeshi la polisi linatoa ovyo kali kwa wote wanaojihusisha na vitendo hivi kuacha mara moja, misako itaendeshwa kwenye maeneo mbalimbali nchini na kwenye mipaka yetu kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika, ili kuwakamata wote wanaojihusisha na biashara hizi na kuwafikisha kwenye vyombo vya Sheria,”alisema kamishina. 

Sanjari na hilo alisema kuwa, lipo suala la  biashara  za magendo  maeneo ya mipakani ambako kumekuwa  na tabia  ya baadhi ya wafanyabiashara kujihusisha na biashara hizo.

Akizitaja biashara hizo, alisema ni uwepo wa uingizwaji holela wa Dawa za  binadamu, dawa za mifugo, kilimo na bidhaa za  vyakula bila kukaguliwa na Mamlaka husika na kutoa onyo kwa wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja.

 Katika hatua nyingine  Kamishina Wakulyamba alisema kuwa hali ya nchi kwa ujumla ni shwari ambapo takwimu zinaonyesha kuwa baadhi makosa kama vile ajali za barabarani zimepungua kutoka ajali 202 zilizotokea Disemba 2019 hadi 133 zilizotokea Mwezi Disemba 2020 ikiwa ni upungufu wa ajali 69 sawa na asilimia 34.  Hata hivyo, aliwapongeza  na kuwashukuru wananchi ambao walishirikiana na Jeshi la Polisi kutii Sheria bila shuruti.