NA JOSEPH NGILISHO ARUSHA

JESHI la polisi Mkoani Arusha, limewaua kwa kuwapiga risasi watu wawili wanaodaiwa kuwa majambazi sugu waliokuwa wakitafutwa kwa muda mrefu kuhusiana na matukio ya uhalifu wa kutumia silaha.

Tukio hilo limetokea mapema majira ya saa sita mchana katika mtaa wa Manyara kata ya Sombetini ,jijini hapa baada ya majambazi hao kukutwa wamejificha katika nyumba moja ya makuti inayouzwa pombe za kienyeji.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, Prosper Maprosoo Mkazi wa Esso, alimtambua jambazi mmoja kwa jina moja la Majengoo ambapo alisema kuwa siku moja kabla ya kuuawa alimpiga risasi mwendesha bodaboda anayeitwa 

Joshua shinga baada ya kumnyima kiberiti.

“Hawa majambazi Jana walitukuta kwenye kijiwe Cha pikipiki wakiwa wawili mmoja mfupi na mwingine mrefu mweupe ambapo yule mweupe alimfuata dereva toyo anaitwa Joshua na kumtaka ampatie kiberiti na alipomwambia hana alimwekea bastola kichwani na baadaye alimfyatulia risasi na kumjeruhi”alisema shuhuda

Aliongeza kuwa majeruhi huyo wa risasi kwa Sasa amelazwa katika hospital ya Mkoa Mount Meru kwa matibabu zaidi.

Naye shuhuda mwingine Emmanuel Mollel Mkazi wa Matejoo alisema kuwa wanalishukuru Jeshi la polisi kwa kufanikisha kuwaua majambazi hao waliokuwa wakisumbua wananchi kwa uporaji wa kutumia mapanga na silaha ya moto aina ya bastola.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha ,Salumu Hamduni, amethibitisha tukio hilo na kusema kuwa atatoa taarifa zaidi hapo baadaye.

Majambazi hao waliokuwa na bastola moja na miiili yao imehifadhiwa katika hospital ya Mkoa Mount Meru kwa ajili ya uchunguzi zaidi.