WASHINGTON,MAREKANI

WAZIRI wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo ameituhumu Iran kwa kuwa na ushirikiano wa kisiri ya mtandao wa al-Qaeda.

Kutokana na madai hayo, Pompeo aliwawekea maofisa kadhaa wa Iran vikwazo.

Kwenye hotuba yake kwa waandishi wa Habari, Pompeo aliishutumu Iran kwa kuwa na uhusiano wa siri na al-Qaeda huku akitaja duru za ujasusi zinazodai kuwa Iran ilimhifadhi kiongozi wa pili wa mtandao huo Abu Muhammad al-Masri ambaye aliuawa mwezi Agosti na mawakala wa Israel.

Kauli ya Pompeo ilikuja wiki moja tu kabla ya utawala wa Trump kuondoka ofisini, na inaonekana kulenga nia ya rais mteule Joe Biden kuanzisha mazungumzo na Iran kuhusu makubaliano ya mwaka 2015 ya mpango wa nyuklia.

Rais Donald Trump aliiondoa Marekani kwenye mkataba huo mwaka 2018.