PARISI, Ufaransa
MABINGWA wa Ufaransa, Paris Saint Germain, wanaendelea na mpango wa kumsaini kiungo wa England na Tottenham Hotspurs, Dele Alli kwa mkopo.
Taarifa kutoka nchini England zinaeleza, maofisa wa PSG wapo jijini London wakiendelea na mazungumzo, lakini, uongozi wa Spurs wameonesha kutokua tayari kumuachia pasipo na kufanikisha harakati za kumpata mbadala wake.
Klabu hizo mbili zimekuwa kwenye mazungumzo kwa siku kadhaa, na dhamira kubwa ya PSG ni kutaka kumpeleka kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 kwa meneja wake wa zamani, Mauricio Pochettino aliyekabidhiwa benchi la ufundi huko Parc des Princes.
Christian Eriksen, ambaye amekuwa na wakati mgumu tangu alipojiunga Inter Milan akitokea Spurs, amekua chaguo la kwanza la Jose Mourinho, katika hatua za kuziba nafasi ya Alli, lakini wababe wa Milan wamewasilisha ombi la kuzuia jukumu la kumlipa mshahara, katika kipindi chote ambacho atarejea England kwa mkopo.(Goal).