Jamii yatakiwa kufanya mazoezi kujikinga na maradhi yasioambukizika

NA MOHAMMED SHARKSY (SUZA)

LEO ni siku ya mazoezi kitaifa hapa Zanzibar ambapo wananchi wote, vikundi vya mazoezi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi katika matembezi yatakayopita kwenye mitaa mbalimbali ya mjini Unguja.

Katika mazoezi hayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ambaye atayaongoza mazoezi hayo yatakayoanzia Mnara wa Mwembe Kisonge kupitia Kwa Biziredi, Mikunguni na kumalizikia uwanja wa Amaan.

Rais wa Zanzibar Dk Mwinyi, ni mara yake ya kwanza akiwa rais kushiriki katika mazoezi hayo ya kitaifa.

Kwa mujibu wa Khamis Ahui Khamis ambae ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha wafanya mazoezi ya viungo Zanzibar (ZABESA) alisema katika mazoezi hayo watu wapatao 3,000 watashiriki kutoka Zanzibar na Tanzania bara.

Aidha alisema jumla ya vilabu 60 vya mazoezi kutoka Unguja na Pemba huku vilabu 20 vikiwa vya watu wenye ulemavu.

Sambamba na hilo, lakini katibu huyo alisema kuwa washiriki kutoka Tanzania bara wapatao 350 kutoka mikoa ya Dodoma, Morogoro, Tanga, Mtwara na Dar es Salaam watahudhuria katika mazoezi hayo.

Katibu huyo alisema ujumbe wa mwaka huu ni ‘Kuimarisha uchumi wa buluu afya kwanza’. Utakaomaanisha namna ya watu kujiajiri katika fursa zinazotokana na uchumi wa buluu.

“Serikali na sekta binafsi pamoja na watendaji wake kwa ujumla wanahamasisha katika kuleta maendeleo makubwa ya kiuchumi kwa kutumia rasilimali za uchumi wa buluu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla”, alisema.

Naibu Katibu huyo aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine lakini lengo la mazoezi hayo ni kuchochea kutoongezeka kwa maradhi yasioambukiza ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa kisukari, moyo, shinikizo la damu na saratani.

“Ni ukweli usiopingika kuwa kwa sasa maradhi yasioambukiza hapa Zanzibar yamekuwa yakiwasumbua watu wengi nah ii inatokana na mfumo mbaya wa ulaji wa vyakula ikiwa ni pamoja na kukosa kula vyakula vya mbogamboga na matunda katika milo ya kila siku”, alisema.

“Kwa kuwa hivi sasa kuna asilimia kubwa ya vifo vinavyotokea duniani ambavyo kwa njia moja ama nyengine husababishwa na maradhi yasiyoambukiza kinyume na miaka ya nyuma na ndio maana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikaona ipo haja ya kuweka siku ya kitaifa ya kufanya mazoezi ambayo vikundi vya mazoezi na watu mmoja mmoja kushajiika kufanya mazoezi bila ya kusubiri siku hiyo ya kitaifa”, anaongeza.

Pamoja na hayo, Khamis alisema kuna umuhimu kwa wasomi kujikita kufanya tafiti za maradhi yasiyoambukiza ambazo zitasaidia kutoa muelekeo na kujua sababu ya kuongeza kwa kiasi kikubwa maradhi hayo.

Hivyo aliomba taasisi husika kutowa elimu juu ya umuhimu wa kufanya mazoezi sambamba na elimu juu ya maradhi yasiyoambukiza ikaanzia kwa wanafunzi maskulini na katika vikundi na mikutano ya kijamii.

Pia kuweko kwa njia za kujikinga na maradhi yasiyoambukiza na tiba yake ili wananchi kuwa na elimu ya kutosha juu ya maradhi hayo.

Sambamba na hilo lakini sasa lazima jamii ijenge tabia ya kutenga muda wa kufanya mazoezi kila siku, kupunguza uzito, kula matunda na mboga mboga kwa wingi vitu vinavyopatikana muda wote nchini na visivyo na gharama kubwa.

“Hivyo tunaiomba jamii kuwa na umuhimu wa kula chakula mchanganyiko chenye lishe kamili kupunguza matumizi makubwa ya mafuta kwa vyakula vya kila siku kwa kuwa yanachangia hatari na chanzo cha kupata magonjwa yasiyoambukizika”, alisema.

NJIA ZA KUFANYA MAZOEZI

Inafaa uanze mazoezi hayo kwa dakika 10 kama mwili wako haujazoea kufanya mazoezi. Polepole, ongeza wakati huo uwe 150.

Ufanyaji wa mazoezi uko wa aina nyingi sana,zifuatazo ni baadhi ya mifano michache ya kufanya mazoezi katika maisha ya kila siku, kama vile Kuruka kamba, Kukimbia, Kucheza ngoma, kupanda milima, kuendesha baiskeli na kuogelea.

Njia nyengine za kufanya mazoezi ni Kucheza mpira wa miguu, mpira wa meza, Kuvuta  kamba,  Kulima kwa kutumia jembe la mkono, kubeba vyuma nakadhalika.

FAIDA ZA KUFANYA MAZOEZI YA MWILI

Mazoezi ni muhimu sana kwa afya ya kiwili wili chako, kila mtu, haijalishi kama mtu ni mnene au mwembamba, mbali na kwamba binadamu tunatofautiana, wote tunahitaji kufanya mazoezi kwa ajili ya afya zetu.

Mazoezi ya kila wakati yanatusaidia kujikinga na maradhi yasiopewa kipaumbile (non communicalble diseases kama vile maradhi ya, Mshituko wa moyo, kiharusi, mfadhaiko.

Aidha mazoezi hupunguza uwezekano wa kupata Shindikizo la damu, mazoezi husaidia kupunguza au kuzuiya uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari.

Sambamba na hilo lakini mazoezi hupunguza uzito, kunyoosha na kuimarisha misuli ya mwili, mazoezi husaidia mapigo mazuri ya moyo kwa kuongeza kasi ya mapigo yake wakati wa mazoezi.

Pia magonjwa ya maungio ya mifupa na kuvunjika kwa mifupa, mazoezi husaidia mmomonyoko wa chakula ambao husaidia kupunguza magonjwa ya kensa   kama vile kensa ya utumbo mpana au matiti.

Mazoezo humfanya mtu kutopoteza  kumbukumbu, husaidia binadamu katika kuurtubisha mfumo wa usagaji chakula kuwa mzuri na uhakika na kupeleka sehemu inyohusika kwa muda muafaka

Aidha mazoezi huimarisha mifupa ya mwili na kukufaya ujisikie mchangamfu na mwenye afya njema, pia hukufanya kujisikia na afya njema kukupa nguvu na kuweza kufanya kazi kwa nguvu zako bila kujisikia umechoka na mwisho wa siku hupunguza mafuta mwilini.

Pia mazoezi husaidia kupunguza mafuta mwilini kama lehemu, ambapo pia huongeza chembe chembe yekundu kwenye mzunguko wa damu ambazo zinabeba oksijen kwenye mapafu na peleka sehemu nyingine za mwili.

Inashauriwa kwamba kwa mtu mzima mwenye afya njema anatakiwa  apate mazoezi yasiyopungua saa 2-1/2 kwa wiki, mazoezi ya nguvu kiasi ya kuongeza mapigo ya moyo.

Aidha binaadamu lazima apate mazoezi ya nguvu ya kuongeza mapigo ya moyo  yasiyopungua saa 1-1/4 kwa wiki au mchanganyiko wa mazoezi ya nguvu na ya nguvu kiasi.

Lakini watu wengi huhitaji zaidi ya saa 2-1/2 kwa wiki ili kuweka miili yao kwenye uzito unaotakiwa.

Aidha Kutembea kwa mwendo wa haraka kwa nusu saa, siku tano kwa wiki, kufanya jogging kwa nusu saa kwa siku, ni baadhi ya mazoezi haya. Yafaa vile vile kufanya mazoezi ya kukomaza misuli angalau mara mbili kwa wiki.

Namna ya kujilinda wakati wa kufanya mazoezi, fanya mazoezi mepesi kabla na baada ya zoezi lako kuu ili mwili upate joto kwanza na uweze kutulia baada ya mazoezi na uendelee kunywa maji kwa wingi ili kurutibisha mwili wako.

Ili kujiepusha na magonjwa mbalimbali ipo haja kuanzia sasa kwa wale ambao hawafanyi mazoezi kutenga angalau muda wa nusu saa kwa siku kuafaya angalau mazoezi katika njia nilizozitaja hapo juu.