NA MWAJUMA JUMA
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) limetuma salamu za rambi rambi kwa familia ya Haji Sultan Temba ‘Haji Kaka’ aliefariki dunia jana.
Haji kaka ambae alikuwa ni Rais wa Chama cha Nage na Mjumbe wa Kamati ya soka la Wanawake, alifariki jana katika Hospitali ya Mnazimmoja alikokuwa amelazwa baada ya kuuguwa kwa muda mfupi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika Shirikisho hilo ambayo imesainiwa na rais wake Seif Kombo Pandu imeeleza kuwa imepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kifo cha marehemu huyo ambae alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya michezo.
“Kwa niaba ya ( ZFF), natoa pole kwa Kamati ya Soka la Wanawake (ZFF), ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu cha msiba”, alisema Rais.
Aidha rais huyo alichukuwa fursa hiyo kuwaomba ndugu , familia na wadau wa soka la Wanawake Zanzibar na wanamichezo wote wa nage kuwa na subra, uvumilivu kwa kuondokewa na mpendwa wao huyo.
“Marehemu Haji Sulatni “Haji Kaka” alikuwa na mchango mkubwa kwa kipindi alichokuwa mjumbe wa kamati ya soka la Wanawake, tutamkumbuka kwa mema yote ambayo ameyafanya”, ilisema Taarifa hiyo.
Mrehemu ameacha kizuka mmoja na mtoto mmoja na amesafirishwa kwao Mkoani Morogoro na atazikwa leo.