NA ABDI SULEIMAN

RAIS wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Seif Kombo Pandu, amekutana na viongozi wa vilabu vinavyoshiriki ligi daraja la kwanza kanda ya Pemba kwa lengo la kujadili mustakbali wa kuanza kwa ligi hiyo msimu huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho katika viwanja vya michezo Gombani, Kombo alisema lengo la kikao hicho ni kusikiliza matatizo na malalamiko ya vilabu hivyo na kuona vipi watatatua changamoto za mpira zilizopo kisiwani Pemba.

Alisema kulikua na sintofahamu nyingi pamoja na baadhi ya miongozo kwa upande wa Pemba haikua vizuri, hali iliyopelekea kukutana na viongozi hao.

Aidha Seif Kombo alifahamisha kwamba ZFF ni shirikisho la mpira na msimamo wake mpira uchezwe kwa vyovyote vile, hata kama kuna baadhi ya vitu vimekosewa ni jukumu lao kuviweka sana au kuvisawazisha ili kuona mpira unachezwa.

Kuhusu ofisi na uwepo wa akaunti ya ZFF Pemba, Kombo alisema haiwezekani kwani chama ni kimoja na kinapaswa kuwa na akaunti moja tu, wakati matawi ya benki yapo maeneo yote, Pemba Chake Chake na Wete.

“Nahitaji tathmini ya kina ni vilabu vya daraja la kwanza zaidi wanazungumzia kumuondoa Rais, sababu za msingi hazionekani ila atajaribu kufanya kukutana tena”alisema.

Hata hivyo aliwataka wadau wa mpira kwamba hayo ambayo wanayasikia kutafufa chanzo chake ili kuelewa kilichopo ni kitu gani, huku akitolea mfano viongozi wa bodi ya ligi.

Aidha aliwaomba wadau wa mpira kutambua kuwa ZFF imeandaa kanuni nyingi zisizopungua saba, hivyo wanapaswa kuzisoma na kuzifahamu ili kuona wanatakiwa kuishi maisha gani katika kuendeleza mpira wa Zanzibar, pamoja na kuona ndani ya wiki moja ligi inaanza.

Kwa upande wake Mohamed Kishore akizungumza katika kikao hicho, alisema awali hawakua na msimamo zaidi, bali waliweza kumueleza vitu ambavyo vipo moyoni mwao na kuona jinsi gani Uongozi wa ZFF unavifanyia kazi.

Alisema ili kutengenezwa mpira wa Zanzibar hakuna budi viongozi wa juu ya ZFF, wanapaswa kukaa pembeni ili kuweze kutengenezwe kwa mpira wa Zanzibar kwa maslahi ya nchi kwa ujumla.

“Sisi tunataka mpira uchezwe na hiyo bodi ya ligi inapaswa kuja Pemba, kuwasilikiliza sisi hatuwezi kucheza mpira kwa misingi ya ubabaishaji, lengo yaliyotokea msimu wa 2019/2020 ligi ilishindwa kumalizika pemba tunataka hilo lisitokee”alisema.

Alisema yote hayo yametokea kutokana na uongozi mbovu wa ZFF, kujimilikisha madaraka yote bila ya kujali mustakbali wa mpira wa Zanzibar.

Hata hivyo alisema vilabu vya Pemba sio kama havitaki kucheza mpira, bali wanahitaji kusikilizwa msimamo wao kama vilabu vya ligi daraja la kwanza.

Hata hivyo baadhi ya wajumbe hao, alisikitisha na kitendo kilicho fanywa na shirikisho hilo kuiridisha tena katika ligi daraja la kwanza kanda ya Pemba, timu ya Majimaji ya Tumbe ambayo miaka mitatu iliyopita haijashiriki katika ligi hiyo baada ya kushushwa daraja.