NA LAYLAT KHALFAN
MKUU wa Mkoa Mjini Magharibi Unguja, Idrissa Kitwana Mustafa, amesema sherehe za mwaka huu za Mapinduzi Matukufu ya 1964 zitakuwa na mtindo wa kipekee ambao haujawahi kufanyika.
Mkuu huyo aliyasema hayo katika viwanja vya Mnazimmoja wakati akizungumza na Mwandishi wa habari wa Zanzibarleo.
Alisema sababu kuu ya kufanya hivyo wamegundua kuwa kuna gharama kubwa zinazotumika kwenye sherehe hizo nabdala yake wameamua fedha hizo kuzipeleka kwenye huduma za kijamii kama vile vituo vya Afya, Elimu, Maji, Miundombinu na mambo mengine yanayofanana na hayo.
Aidha, alifahamisha kuwa, dhamira yao ni kuona namna gani Mapinduzi hayo yanaakisi upatikanaji maendeleo kwa wananchi katika kutoa huduma bora na muhimu zilizokusudiwa badala ya gharama hiyo kufanyiwa sherehe.
Kitwana alisema katika maeneo mengi yanayotolewa huduma za wananchi, imebainika kuwa upatikanaji wa huduma hizo unakuwa ni wakusua sua huku ukizingatia wananchi wamekabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinahitaji kutafutiwa ufumbuzi.
Alisema kwa kawaida sherehe hizo zimezoeleka kila ifikapo Januari 12 kufanyika katika viwanja vya Amani lakini mwaka huu zitafanyika katika uwanja wa Mnazi Mmoja huku kukiwa na shamra shamra mbalimbali ikiwemo maandamano ambayo ndio alama kubwa ya Mapinduzi hayo.
Aidha, Mkuu huyo ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya sherehe hizo, alisema kutokana na sababu hiyo ndani ya mwaka huu watapunguza baadhi ya mialiko ambayo imetajwa kuwa ndio miongoni mwa kupunguza gharama hizo.
Alieleza kuwa, utaratibu utakaotumika mwaka huu unaweza kuwashawishi katika miaka mengine inayokuja kwa kuendelea nao haijalishi hata kama watafanyia katika viwanja vya Amani.
Aidha, aliwataka wananchi kutosita kufika katika kusherehekea siku hiyo huku wakiwa na matumaini makubwa na serikali yao ya awamu ya nane katika kuona yale maendeleo kuanza ndani ya sherehe hizo.