ZASPOTI

Anamiliki dola za kimarekani milioni 600

ROBYN Rihanna Fenty, maarufu kama Rihanna, ni mwimbaji wa Kimarekani, ambae ameanza kujulikana mnamo mwaka 2005, baada ya kutoa wimbo wake ‘Music of the Sun’ na miaka ya mbele kuachia vibao vilivyozidi kumtambulisha ulimwenguni kama ‘Umbrella’, ‘Diamonds’ na ‘Rude Boy’.

Rihanna aliezaliwa Februari 20, 1988 huko Saint Michael, Barbados anaejulikana ulimwenguni kwa muziki wake wa ‘POP’ na ‘R&B’ amezidi kuuteka ulimwengu kwa sauti yake ya kipekee, umahiri wa kuimba na kutamba juu ya steji pamoja na mitindo yake.

Mbali na kipaji chake cha muziki, mnamo mwaka 2006, Rihanna alijiingiza katika fani ya uigizaji na kuigiza filamu mbali mbali kama vile ‘Battleship’, ‘Bring It On: All or Nothing’, ‘Valerian’ na ‘Ocean’s 8’, ambazo zilizidi kuonesha umahiri wake na wengi kuvutiwa nae.

Aidha mnamo mwaka 2010, Rihanna aliingia kwenye biashara, ambapo alizindua bidhaa yake ya kwanza ambayo ni manukato aliyoyaita, ‘Reb’l Fleur by Rihanna’.

Sambamba na hilo mnamo mwaka 2017 alianzisha kampuni yake ya vipodozi inayoitwa ‘Fenty Beauty’ ambapo bidhaa zake kama vile rangi za midomo, poda, zilipata umaarufu sehemu nyingi duniani, ambapo takwimu za mwaka 2018 zinaonesha kampuni hiyo ilikusanya dola za kimarekani milioni 570.

Mnamo Mei 2019, chapa ya kifahari ya Ufaransa ‘LVMH’ ilithibitisha itazindua kampuni ya mitindo ya Rihanna, Fenty, na kumfanya kuwa mwanamke wa kwanza mwenye rangi kuongoza kampuni hiyo ya mitindo.

Kwa mujibu wa taarifa za ‘Forbes’, LVMH pia inaunga mkono kampuni ya vipodozi yenye faida kubwa ya Rihanna ‘Fenty Beauty’.

Kwa mujibu wa Jarida la ‘Forbes’, Rihanna ametajwa kuwa ni mwanamuziki wakike aliyeshika nambari moja ya utajiri ulimwenguni ambae anamiliki kiasi cha fedha za kimarekani milioni 600.

Akifuatiwa na mwanamuziki Madonna anaemiliki fedha za kimarekani  milioni 570, Celine Dion milioni 450 milioni, Beyoncé na Barbra Streisand milioni 400 na Taylor Swift milioni 360.

Kwa mujibu wa jarida la Forbes utajiri wote huo ni kutokana na kazi zake za muziki, biashara pamoja na mapato yaliyopatikana kutoka kwa mitindo yake na urembo na sio wa kurithi.

Chapisho hilo linafafanua kuwa”Rihanna amejitengeneza yani kama mtu aliyejenga kampuni au kuanzisha utajiri kwa nguvu zake  badala ya kurithi”.

Rihanna aliiambia ‘New York Times’ kwamba hatoendeshwa na pesa bali na kazi yake, “Fedha hizo zinamaanisha kuwa ninaweza kutunza familia yangu, fedha pia inamaanisha kuwa naweza kuwezesha biashara ninazotaka.

Aidha alisema anaweza kumsaidia kazi mtu mwengine kwa kupitia fedha zake “siku zote ninawaza kwamba kupitia fedha zangu naweza kumsaidia mtu mwingine au kuzitumia kwa watoto wangu katika siku zijazo” alisema.

Mnamo mwaka 2012, Rihanna alianzisha ‘Clara Lionel Foundation’, ambayo inasaidia juhudi za afya na elimu katika jamii masikini ulimwenguni.

Pia mnamo Februari mwaka 2017, Chuo Kikuu cha Harvard kilimtaja kuwa ni muhisani mkubwa duniani katika masuala ya kibanaadamu wa mwaka.

Rihanna amemtaja mwanamuziki mashuhuri Madonna kama mtu anaemtia ushawishi na hamasa kubwa katika tasnia ya muziki.

Alisema kuwa alitaka kuwa “Madonna mweusi” na akamsifu mwimbaji huyo kwa kuweza kujiboresha mara kwa mara kimafanikio katika kazi zake zote.

Alibainisha kuwa “Nadhani Madonna alikuwa msukumo mkubwa kwangu, haswa kwenye kazi zangu za mwanzo”.

Ukimzungumzia Rihanna katika suala zima la muziki basi basi huwachi kutaja, mabadiliko ya muziki, nitindo na hisia za uimbaji ambayo yamepelekea kuvishika vyombo vya habari.

Katika mahojiano na jarida la ‘Look’, Rihanna alizungumza juu ya kulinganishwa na Beyonce, “Beyonce ni msanii mzuri na ninajisikia kuheshimiwa kutajwa katika sentensi hiyo hiyo, lakini sisi ni wasanii tofauti na mitindo tofauti”.alifafanua.

Miaka yake katika muziki imemfanya kuwa kiungo wa ‘pop’ na mwimbaji mwenye ushawishi mkubwa katikia tasnia ya sanaa.

Mpaka Septemba 2018, Rihanna ameuza zaidi ya rekodi milioni 250 ulimwenguni, na kumfanya kuwa mmoja wa wasanii wa muziki wanaouzwa zaidi.

Katika kazi zake zote, amepokea tuzo mbali mbali miongoni mwao, tisa za Grammy, 12 za muziki wa Billboard, 13 za muziki wa marekani, nane za Chaguo la Watu.

Nchini Marekani, Rihanna ameuza zaidi ya Albamu milioni 10, wakati Nielsen SoundScan alimuweka kama msanii wa kisasa anaenunuliwa zaidi nchini humo.

Kwa mujibu wa kampuni ya kurikodi ‘Guinness’, Rihanna amevunja Rekodi ya Ulimwengu ya kwa mauzo ya zaidi ya milioni 58 kufikia mwaka 2012.

Huko Uingereza, ameuza zaidi ya Albamu milioni 7, na kumfanya kuwa msanii wa tatu wa kike anayeuzwa zaidi katika karne hii.

Kulingana na Billboard, jumla ya mauzo yake ya albamu yapo nakala milioni 54 kuuzwa ulimwenguni.

Ukizungumzia suala zima la mahusiano, Rihanna alikua na mahusiano na Chris Brown Mwimbaji mashuhuri wa kimarekani ambae walijuana tangu mwaka 2005 na walidumu kwenye uhusiano hadi mwaka 2009.

Mapenzi yao yalikatika baada ya mabishano kati ya wenzi hao kuongezeka kwa Brown kupata vurugu na Rihanna, na kumuacha na majeraha ya mwili.

Mnamo mwaka huo huo wa 2009 uvumi juu ya uchumba wa Rihanna na mwanamuziki wa kimarekani Drake Graham ulizunguka kwa miaka kadhaa kutokana na ushirikiano kadhaa kati ya wasanii hao wawili.

Wakati wa mahojiano yake na ‘Hot-97’, Rihanna alitangazwa kuweka wazi juu yake na Drake akijaribu kimapenzi, lakini wakati huo tu akabadili kauli.

“Kwa kweli nilivutiwa na Drake, lakini nadhani ndivyo ilivyo, kama ilivyokuwa hatukutaka kuipeleka mbali zaidi ilikuwa wakati mgumu sana maishani mwangu, kwa hivyo sikutaka kuwa mbaya kwa mtu yeyote wakati huo” alisema.

Drake pia alifunguka juu ya uhusiano huo mfupi, akiambia ‘The New York Times’ kuwa “Alikuwa akifanya haswa kile nilichowafanyia wanawake wengi katika maisha yangu yote ambayo ni kuwaonyesha wakati mzuri, kisha kutoweka”, alisema.

Huyo ndie mwanamke mashuhuri na tajiri kutokana na kazi yake ya Sanaa ambayo imempa umahiri mkubwa.