Ajipanga kutimiza ndoto ya kuanzisha kituo kulea vipaji
NA ZAINAB ATUPAE,ZASPOTI
“NDOTO zangu ni kuwa na kituo kikubwa cha kulelea na kukuza vijapaji vya mpira wa miguu kwa vijana wanawake ambacho kitatoa timu za madaraja mbali mbali”.
Hayo ni maeno ya kocha wa timu ya wanawake ya ‘New Ganaration’, Riziki Abubakar Islaha, ambae alizaliwa mwaka 1989 huko Makadara wilaya ya Mjini Unguja.


Riziki ametokea kuwa nyota anayetajikana katika visiwa vya Unguja na Pemba na hata katika mikoa ya Tanzania Bara na nje ya nchi, akiwa mchezaji mzuri wa mpira wa miguu.
Hii ni kutokana na historia yake kuanza kuvuma tangu akiwa mtoto wa miaka 10 pale alipojiingiza katika timu ya mpira wa miguu ya wanaume iliopo katika mtaa wao, akiwa ni mwanamke pekee.

SAFARI YAKE KIMCHEZO
Riziki aliupenda mchezo huo, akichezea namba 10 akiwa ni kiungo mshambuliaji au winga mwenye uwezo wa kufunga magoli na anacheza kama mshambuliaji wa kati ingawaje si mshambuliaji halisi.


Muda mwingi Riziki akiwa anachezea sehemu hiyo huwa hakai sehemu moja kusubiri mipira kama ilivyo kwa ‘kawaida ya NO. 9’ na huzunguka kulia, kushoto na katikati kujaribu kutafuta mipira ili aweze kufunga.


Tangu aanze kuichezea nafasi hiyo ameonekana anayeimudu vyema kazi yake hiyo, kwani akiwa uwanjani aliweza kuwafanya mashabiki wake kutotulia katika viti vyao, na kubaki kumpigia mayowe ya kumshangiria kwa kazi yake nzuri anayoifanya.


Wakati mwengine, Riziki akiwa uwanjani huonyesha mbwembewe kama vile walizonazo wachezaji wa kimataifa hiyo inatokana na kuumudu vyema mpira wa miguu kiasi ambacho umemfanya kuwa ni sehemu ya maisha yake kiasi ambacho ameiweka kama starehe yake anayoipenda maishani mwake.


Hii ndio iliyomfanya hadi leo, kubakia kuwa mchezaji mzuri wa nafasi yake hiyo ya kuwa kiungo mshambuliaji kiasi ambacho kimechangia kumfanya hadi sasa kuwa nyota inayotamba kwa mpira wa miguu visiwani Unguja na Pemba.
Mwaka 2008, akiwa na miaka 19 alianza kuichezea timu ya New Generation, ambayo iliyoundwa na wanawake ambayo hadi sasa anaendelea kukuitumikia akiwa kama kocha mchezaji.


Mshambuliaji huyo alizaliwa mwaka 1989 huko Makadara Mkoa wa Mjini Unguja, na kuendelea kuishi na familia yake akiwa ni mtoto wa kwanza, kwani wapo wanne akiwemo mwanamme mmoja na wanawake watatu na aliishi mtaa huo hadi pale alipoolewa.

MAISHA YAKE YALIVYOKUWA
Akizungumzia maisha yake, alisema alianza kusoma mwaka 1997 ambapo darasa la kwanza hadi la saba katika Skuli ya Muembeshauri, na kumaliza mwaka 2003, ambapo mwaka 2004/2005 aliendelea Sekondari Heileselasie kuanzia darasa la nane hadi la tisa na kuondoka Skuli hiyo.


Alisema 2006-2007 alibahati kuondoka na kwenda nchini Uganda huko aliendelea kusoma kuanzia darasa la 10 hadi 11 katika Skuli ya Happy Haurs Senior Secondary School na baada ya kumaliza masomo alirudi nchini kuendelea darasa la 12 na alihitimisha elimu yake katika Skuli ya Lumumba.


Wakati akiendelea na masomo baada ya kumaliza ndipo uhondo wa kucheza mpira anasema ulimkolea, huku akiendelea kufanya biashara zake ndogo ndogo zinazompatia riziki katika maisha yake.
“Nilipomaliza kusoma na nilipona kuwa napenda mpira tokea mdogo nikaamua kuendeleza kipaji changu nikawa nacheza na watoto wenzangu wakiume nikasema ipo siku na mimi nitaonekana” alisema.


“Familia yangu ni ya kawaida na tunashukuru ambacho tunakipata katika maisha yetu ya kila siku”, alisema.
Riziki akizungumzia suala la michezo alisema amekuwa akiipenda na ndio maana aliamua kujiunga na timu hiyo ya New Generation baada ya kuiona iko vizuri licha ya kupata changamoto ya kukosa mashindano, lakini inapokuwepo ligi ya wanawake huwa inafanya vyema.


“Mimi sikuwa na timu nyingi ambazo nimecheza, lakini, kama nilivyokuambia kuwa nilicheza timu za watoto hadi nilipopata nafasi ya kusajiliwa katika timu hiyo na nikaanza kucheza soka na ndipo nilipopata nafasi ya kutangaza kipaji changu hadi leo”,alisema.
Alisema timu yao bado iko vizuri kwan ina ushindani, na anaamini watafanya vyema katika ligi kuu wanayoshiriki.
Wakati akiwa na timu yake hiyo, Riziki, alisema kwamba alifanikiwa kucheza na wachezaji wengi, akiwemo Nafisa Muharam ambae alikuwa akicheza namba tano, Fatma Omar ambae kwa sasa ni kocha wa makipa wa timu ya Taifa Tanzania ya wanawake.

CHANGAMOTO

Pia, akizungumzia juu ya changamoto ambazo wanazipata katika soka la wanawake, ni kushindwa kupewa thamani kama wanavyopewa timu za wanaume.
Sambamba na hayo hakuacha kuzungumzia juu mwenendo mzima wa ligi ambapo, alisema vipaji vya wanawake vipo, lakini, Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), bado hawajakuwa tayari kutoa vipaji hivyo ambapo wanaangalia kwa ligi za wanaume pekee.

NINI KIFANYIKE KUKUZA SOKA

Riziki anasema katika kukuza soka Serikali ya Zanzibar na ZFF, zione umuhimu wa kuwapa kipau mbele kufuatilia soka la wanawake, kwani imeonekana hali haiko vizuri kwani hata ligi wanaiendesha katika mazingira magumu.


Jambo jengine ambalo Riziki amelisema ni kwa serikali, kuona umuhimu wa kuweka fungu la timu za wanawake katika Wizara inayoshughulikia masuala ya Michezo na kuhakikisha linawafikia wahusika wenyewe.


“Fungu la wanawake linawekwa kwa tunavyosikia, lakini inakuwa ngumu kuwafikia wahusika na tunacheza ligi kwa hali ngumu hiyo miaka ambayo ligi inachezwa”,alisema.
Riziki anasema katika kutaua changamoto hizo, ni vyema Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), kuwa na programu ya kuhamasishaji viongozi, ili mpira wa wanawake kupata soko na thamani ili iwe kama ligi ya wanaume kwa kuifanya jamii kuchukulia mpira wa wanawake kama kazi nyengine na kuacha tabia ya kuwadharau.


Alisema hiyo ni kutokana na kuonekana jamii haina muamko kwa kushindwa kutambua kazi ambayo wanaifanya vijana wanawake, huku wakiwambia kuwa mpira sio uhuni kama wanavyosema wao.
Alisema tatizo la kukosa elimu ya soka la wanawake kwa wachezaji wenyewe na jamii bado nalo ni kikwazo kwani wengi wao waoana halina msingi jambo ambalo linasababisha kukosekana kwa mwamko wa soka hilo.

“Tuseme ukweli ujue tokea mwaka 2017 tulipomaliza ligi hadi leo hatujacheza tena na tunataka kucheza mwaka huu utasema kuna muamko wa soka la wanawake ambapo ligi ya wanaume kila mwaka inachezwa”,alisema.