MILAN, Itali

MSHAMBULIAJI wa Juventus, Cristiano Ronaldo amesema hana mpango wa kustaafu soka hivyo ataendelea kucheza kwa miaka mingi zaidi licha ya kukaribia umri wa miaka 36.

Ronaldo raia wa Ureno msimu wa 2020/21 ametupia kambani mabao 16 kwenye mechi 14 alizocheza katika mashindano yote, huku 12 akifunga kwenye ligi ya Serie A.

Ronaldo atakuwa na umri wa miaka 36 ifikapo mwezi Februari 2021 ana mkataba na timu ya Juventus hadi ifikapo mwaka 2021 na amesema anataka kusakata kabumbu hadi akitimiza umri wa miaka 40.

 Wakati huo huo mwanasoka huyo amezidi kuandikisha historia na kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kama mtu wa kwanza duniani kufikisha wafuasi milioni 250 katika mtandao wa Instagram.

Ronaldo hivi karibuni alijinyakulia tuzo ya mchezaji bora wa karne hii.

Nyota huyo aliyewahi kuzichezea Manchester United na Real Madrid, sasa yupo nchini Italia akikipiga na Juventus ambayo inafanya vizuri na imekua ikitegemea huduma zake.