NA TATU MAKAME

ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya kaskazini ‘A’ Unguja, Hassan Ali Kombo, amesema kukosekana kwa hati miliki kwa baadhi ya wananchi wanaomiliki ardhi ndani ya wilaya hiyo ndio chanzo cha migogoro ya ardhi.

Hassan alisema hayo Ofisi za Wilaya Gamba, Mkoa wa Kaskazini Unguja, wakati akimkabidhi Ofisi Mkuu wa wilaya hiyo Sadifa Juma Khamis, ambapo alisema wananchi wengi wa Wilaya hiyo wananunua na kuuza ardhi, bila kuwa na hati miliki ya ardhi hali inayoleta migogoro katika jamii.

Alihamisha kuwa kesi nyingi zilizofika ofisini kwake ndani ya uongozi wake ni malalamiko ya ardhi ya wananchi kulalamikia kunyang’anywa ardhi zao huku wengi wao wakiwa hawana hatimiliki hali inayoleta ugumu katika kutoa maamuzi.

Hata hivyo, alimtaka mkuu mpya wa Wilaya kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo, kwa kuhakikisha kila mwananchi anaemiliki ardhi anakuwa na hatimiliki yake kuondosha tatizo hilo kwa wananchi atakaowaongoza.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Sadifa Juma Khamis, aliwataka watendaji kuwa na umoja na mshikamano sambamba na kuongeza uwajibikaji katika kazi, ili kuondoa kero zinazo wakabili wananchi.

Aidha aliahidi kulifanyia kazi tatizo la migogoro ya ardhi kwa kushirikiana na masheha wa shehia husika ambazo hulalamikiwa, ili kupata ufumbuzi juu ya kadhia hiyo.

Nao wananchi wa Wilaya hiyo walisema kesi nyingi husababishwa na viongozi wa juu ambao hufika maeneo yanayomilikiwa na wananchi kuchukua ardhi kwa nguvu na kujimilikisha au kuweka vitega uchumi ikiwemo kujenga mahoteli.