NA ASYA HASSAN

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa tamasha la saba la biashara linalotarajiwa kufanyika katika viwanja vya Maisara wilaya ya Mjini Unguja. 

Tamasha hilo linalotarajiwa kufunguliwa Januari 6 ya mwaka huu litashirikisha wajasiriamali na wafanyabiashara wakubwa kutoka ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania. 

Akizungumza na vyombo vya habari katika viwanja vya Maisara, kaimu waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Mudrik Ramadhan Soraga, alisema lengo la kufanyika kwa tamasha hilo ni kusherehekea maadhimisho ya sherehe za mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.

Soraga alifahamisha kwamba kufanyika kwa tamasha hilo kunaleta mafanikio kadhaa ikiwemo kuongeza pato la serikali kwa kuweza kupata fedha ambazo zinasaidia katika kuihudumia jamii katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo.

Aidha alisema kufanyika kwa tamasha hilo ni chachu kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wakubwa kutangaza biashara na bidhaa zao pamoja na kupata masoko ya uhakika.

“Tamasha hili hutoa fursa kwa wafanyabiashara, wenye viwanda, taasisi za serikali pamoja na taasisi binafsi hutumia nafasi hiyo kutangaza biashara au huduma wanazozitoa kwa watembeleaji tamasha hilo,” alisema.

Hata hivyo waziri huyo alifahamisha kwamba maonyesho hayo pia yanasaidia ukuwaji wa sekta ya biashara kutokana na sekta hiyo ni muhimu na chanzo cha kuongeza ajira na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na kuongeza pato la taifa.

Sambamba na hayo alisema kupitia tamasha hilo pia kutakuwa na vitu mbalimbali ikiwemo kuwepo kwa jukwaa maalum la kutangaza uchumi wa buluu pamoja na kuwa na siku ya ubunifu yenye lengo la kuibua vipaji vya wajasiriamali katika maeneo ya mashine na teknolojia ya habari.

Alifahamisha kwamba hatua hiyo itasaidia kwa wajasiriamali hao kuweza kujiajiri na kuchochea utendaji kazi katika viwanda vidogo vidogo na na vya kati pamoja na kutangaza huduma au bidhaa mpya zilizoanza kuingia sokoni.

Akizungumzia mafanikio ya tamasha la sita lililopita waziri huyo alisema tamasha hilo liliweza kutoa mafanikio kadhaa ikiwemo wafanyabiashara na wajasiriamali kuuza bidhaa zao kwa asilimia kubwa na kuwaongezea kipato.

Waziri huyo pia alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi kwenda kutembelea katika tamasha hilo ili waweze kuipata huduma mbalimbali pamoja na kununua bidhaa tofauti kwa lengo la kuwaunga mkono wajasiriamali na wafanyabiashara watakaofika katika eneo hilo.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Biashara na Masoko Khamis Ahmada Shauri, alisema maandalizi ya tamasha hilo yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 90, hivyo alivisisitiza vyombo vya habari kuendelea kulitangaza ili liweze kufahamika zaidi pamoja na kusaidia kuikuza sekta ya biashara.

Alisema wizara hiyo imekuwa ikifanya tamasha hilo kila mwaka ili kuisaidia serikali katika kuikuza sekta hiyo pamoja na kuchochea maendeleo ya nchi.

Tamasha hilo ambalo linatarajiwa kuanza Januari 4 na kufungwa Januari 15 ya mwaka huu na zaidi ya washiriki 340 wanatarajiwa kushiriki katika tamasha hilo.