MWANADAMU kwa msaada wa teknolojia anajaribu kutaka kuvumbua vitu katika mazingira yote yanayomzunguuka ikiwemo baharini, majini na angani.

Kwa upande wa angani taasisi na mashirika kadhaa yanapeleka vyombo kwenda kugundua mambo mbalimbali yaliyopo angani ikiwemo kutafuta sayari nyengine.

Hivi karibuni kundi wa watafiti kutoka Marekani wamesema wamegundua satilaiti 12 mpya za Jupiter, na hadi sasa satilaiti za sayari hiyo zilizogunduliwa zimefikia 79.

Taasisi ya sayansi ya Carnegie ya Marekani imetoa taarifa ikisema watafiti waligundua satilaiti hizo katika majira ya mchipuko mwaka jana.

Watafiti hao wa kituo cha sayari ndogo cha shirika la wanajimu la kimataifa wamehesabu mizingo ya satilaiti hizo na utafiti huo uliendelea kwa mwaka mzima.

Watafiti wamesema miongoni mwa satilaiti 12 zilizogunduliwa, satilaiti 9 ziko mbali na Jupiter, zinazunguka kinyume na upande unaojizungusha Jupiter na muda wa mzunguko mmoja ni miaka miwili hivi.

Satilaiti mbili ziko karibu na Jupiter, zinazunguka kuendana na upande wa unaojizungusha jupiter, na muda wa mzunguko mmoja haujafikia mwaka mmoja.

Satilaiti nyingine ndogo zenye kipenyo cha kilomita 1 hivi inazunguka katika mzunguko tofauti na ina uwezekano wa kugongana na satilaiti nyingine.

Jupiter ni sayari kubwa zaidi inayojizunguka kwa kasi zaidi kwenye mfumo wa jua, pia ni sayari yenye satilaiti nyingi zaidi kwenye mfumo huo.