NA SAIDA ISSA, DODOMA

SERIKALI imesema inakaa na kuipitia upya  Sheria ya ushirika namba sita ya Mwaka 2013 ili kuona vikwazo vilivyopo inaviondoa ili waweze kuona maendeleo ya ushirika wenye tija.

Hayo yalielezwa  Jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo, DK Adolph Mkenda, wakati wa hafla ya kukabidhi Magari manne pamoja na Kompyuta kwa Tume ya Ushirika nchini.

Waziri Mkenda alisema lengo la kuipitia Sheria hiyo ni kuweza kunyanyua Ushirika Nchini na kuwakomboa Wakulima kwa wanachozalisha.

Sanjari na hilo alisema kuwa hawatawavumilia wezi na wabadhirifu wa Ushirika,  ili kuweza kuondoa wimbi hilo ambalo limeonekana kuwa kubwa.

Aidha alisema lengo la Vyama vya  Ushirika ni kuweza kuwasidia wakulima kunufaika na mazao yao kwa kuwatafutia masoko kwani peke yao hawawezi.

Mrajisi wa Tume ya maendeleo ya Ushirika Tanzania bara, Benson Ndiege, alisema kuwa Tume hiyo imekuwa ikifanya juhudi kutatua changamoto zilizokuwepo awali ikiwemo uongozi mbovu na kushuka kwa maadili ambapo wanaendelea kuhamasisha wanachama wa ushirika  kushiriki kikamilifu katika Vyama vyao.

Awali akitoa neno la Shukrani Naibu Mrajisi wa Tume hiyo ya maendeleo ya Ushirika-udhibiti,Collins Nyakunga alieleza jinsi walivyojipanga katika utendaji kazi na kuahidi kufanya kazi kwa kufuata Sheria na taratibu ikiwa ni pamoja na kutowavumilia wale watakaoenda kinyume na taratibu za Ushirika.

Nao baadhi ya Warajisi ambao wamezungumza na kituo hiki wameeleza umuhimu wa  Sheria itakavyosaidia katika utendaji wa kazi.