NA NASRA MANZI

KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Vijana ,Utamaduni na Michezo Omar Hassan ‘King’ amesema serikali itahakikisha inasimamia riadha ili kurejesha hadhi yake na kupata viwango bora vya wakimbiaji.

Akizungumza mara baada ya kumaliza mashindano ya mbio za kilomita 10 kwa wanaume na wanawake,ikiwa ni shamra shamra za kutimia miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar huko Mnara wa Kumbukumbu Kisonge.

Alisema lengo ni kupata washiriki watakaowakilisha katika mashindano mbali mbali ya kitaifa, pamoja na kuinua viwango vya wanariadha.

Hata hivyo alisema wapo wachezaji ambao wamevunja rikodi katika mbio ,hivyo ni vyema kufanya juhudi za kuibua vipaji zaidi ili kuweka historia mpya.

Pia alisema serikali ya awamu ya nane inatilia mkazo suala la kuimarisha michezo,hivyo kwa upande wa riadha itahakikisha inasimamia katika hali inayotakiwa kuurejesha mchezo huo.

Sambamba na hayo King alisema ili kuhakikisha riadha inaimarika itafufua vipaji vya riadha katika skuli mbali mbali kwa lengo la kuongeza rikodi na kupata viwango na wachezaji bora.

Akisoma risala Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Suleiman Ame Nyambui alisema chama kinakabiliwa na changamoto katika kuendesha shughuli zao ikiwemo wafadhili.

Alisema ukosefu wa viwanja kutokuwa na vifaa vya kutosha katika michezo kwa kufanyia mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Alieleza changamoto nyengine usafiri wa timu ya taifa inapokuwa kwenye maandalizi.

Hata hivyo waliiomba wizara kupatiwa walimu wa michezo kutoka nje ya nchi kama ilivyokuwa miaka ya 70 hadi miaka ya 80.

Jumla ya wanariadha 250 Zanzibar kutoka sehemu mbali mbali wameshiriki mbio za kilomita 10 kwa ajili ya kusherekea miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.