Hemed awanoa vijana wa CCM

NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MJUMBE wa kamati kuu ya halmashauri kuu ya taifa ya CCM, Hemed Suleiman Abdulla amesema vijana wana wajibu kutafsiri kwa vitendo maana halisi ya uhuru wa taifa lao kwa kuleta mapinduzi ya kiuchumi.

Akizindua matembezi ya hiari ya Umoja wa Vijana wa CCM ya kuyaenzi mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 huko katika viwanja vya Burudani Pwani Mchangani yaliyoshirikisha vijana kutoka wilaya zote Zanzibar na baadhi ya mikoa ya Tanzania bara, alisema vijana wana nafasi ya kusaidia mapinduzi ya kiuchumi.

Alisema historia inaonesha kwamba nguvu na ari za vijana ndizo zilizotumika kukomesha ukoloni, hivyo vijana wa kizazi kipya ni muhimu kwao kujitambua na kujiweka imara katika kufanikisha malengo ya ukombozi kwa jamii.

Alifahamisha kwamba endapo vijana wataendelea kushirikiana vyema na kusaidiana katika kutafuta na kutengeneza ajira changamoto zinazowazunguka ndani ya jamii zinaweza kutatuka kwa kiwango kikubwa.

Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alisema serikali zote mbili ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeweka mfumo mzuri wa upatikanaji wa ajira kupitia sekta ya umma na binafsi ambazo humuwezesha kijana kuepuka mambo maovu.

Alieleza kuwa serikali imedhamiria kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa makundi yote ya vijana kwa lengo la kuhakikisha inawapatia fursa za ajira kwa namna iliyo bora na sahihi.

Hemed alilipongeza kundi hilo la vijana  kwa uamuzi wao waliouchukuwa kupitia matembezi hayo ya hiari ya siku nane yatakayojumuisha shughuli tofauti za ujenzi wa taifa na kujijenga katika uzalendo na utii wa kupigania maslahi mapana ya taifa.

Mjumbe huyo wa kamati kuu aliwakumbusha vijana hao kuwa tanuri la kuwafinyanga wenzao mitaani kujiepusha na vitendo vya rushwa, wizi, ubadhirifu na uzembe unaokwaza kufikiwa hatua za maendeleo.

Aliuagiza uongozi wa halmashauri zote lazima uhakikishe unapatikana usalama wa kutosha wa msafara wa vijana hao kila watakapopita na kushiriki katika ujenzi wa taifa.