ZASPOTI
KIUNGO wa zamani wa Al Ahly, Mohamed Shawky, amekuwa nyota wa karibuni kumkosoa kocha mkuu wa sasa, Pitso Mosimane, kwa mbinu zake.
Mashetani wekundu hao hivi karibuni waliteleza kwenye Ligi Kuu ya Misri baada ya kuacha pointi mbili dhidi ya Wadi Degla kufuatia sare ya bila ya kufungana.
Matokeo hayo hayakupokelewa vyema na wachambuzi wengi wa Misri, akiwemo mkongwe wa Ahly, Ahmed Belal, ambaye alikosoa uamuzi mbaya wa Mosimane baada ya mchezo.
Licha ya sare yao, Ahly kwa sasa wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Misri, ikiwa nyuma ya vinara El-Gouna kwa pointi moja huku wakiwa na mchezo mkononi.
Hata hivyo, Mohamed Shawky anaamini utendaji wa Ahly wiki iliyopita unaweza kuathiri matokeo yao chini ya Mosimane katika siku zijazo.
“Sishawishiki na mbinu za Mosimane na Al Ahly,” Shawky aliambia, MBC Masr.
“Hakuna mtu atakayezungumza juu ya matokeo, lakini, hadi sasa, siwezi kuamua mtindo wao wa uchezaji chini ya Mosimane, haujulikani kwangu.
“Ikiwa Ahly wataendelea kucheza vile wanavyofanya, watakabiliwa na shida nyingi na hakika watalazimika kupambana kwenye Kombe la Dunia la Klabu”, akaongeza.
Al Ahly wamepangwa kushiriki Kombe la Dunia la FIFA linalokuja, ambalo limeahirishwa hadi Februari kwa sababu ya janga la ‘corona’.
Shawky anachukuliwa kuwa mmoja wa viungo bora kabisa kucheza huko Ahly, akijiunga na mashetani wekundu hao mnamo Julai 2003 akitokea Al Masry, kabla ya kuondoka kwenda Middlesbrough ya Ligi Kuu ya England wakati huo miaka minne baadaye.
Kisha akarejea Ahly mnamo 2010, kabla ya kuondoka mara moja 2012, lakini, mara hiyo huko Iraqi akiwa na Naft Al-Janoob, kisha Kelantan FA ya Malaysia, na mwishowe akastaafu mnamo 2015 na Arab Contractors.
Katika kiwango cha kimataifa, ana mechi 65, akifunga magoli matano, maarufu zaidi dhidi ya Brazil kwenye Kombe la Shirikisho la 2009, na akainua taji la AFCON 2006 na 2008 akiwa na ‘Mafarao’.(Goal).