NA HAFSA GOLO

HATUA ya kufanyika kwa maadhimisho ya kilele cha sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar mwaka 2021 katika viwanja vya wazi vya MnaziMmoja imelenga kutoa fursa kwa watu wengi kushiriki katika maadhimisho hayo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dk. Khalid Salum Mohamed alieleza hayo alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Vuga kuhusu uamuzi wa serikali juu ya kuadhimisha maadhimisho hayo katika viwanja hivyo.

Alisema kilele cha maadhimisho hayo kufanyika hapo pia kunatoa fursa nyengine ya kushughudiwa na wananchi wa rika tofauti.

Aidha alisema, kufanyika kwa matembezi ya vikosi vya ulinzi na usalama katika barabara zilizopita katika maeneo mbali mbali ya mji ya Zanzibar siku ya kilele hicho nayo yatavutia wananchi na burdani.

Waziri huyo aliongeza kwamba Mapinduzi ya mwaka 1964 ni ya wananchi wote kwani ndio yaliomkomboa Mzanzibari na kuleta usawa na haki kwa wananchi wote bila ya kujali tofauti zao za rangi, kabila, dini na jinsia.

Kwa maana hiyo, Dk. Khalid alisema, kufanyika kwa maadhimisho hayo katika maeneo ya wazi kutasaidia kushiriki kikamilifu kwa wananchi wote pamoja na mambo mengine.

Vile vile alisema, wananchi   walipata fursa nzuri ya kushiriki tamasha la biashara lililoshirikisha wafanyabiashara na wajasiriamali zaidi 327 kutoka Unguja, Pemba, Tanzania bara na nje ya Tanzania.

Dk. Khalid alisema, pia kufanyika kwa kilele hicho viwanjani hapo ni jambo la kihistoria kwani itakumbukwa kwamba mara baada ya Mapinduzi matukufu mwaka 1965 hadi kufikia mwaka 1973 sherehe hizo zilikuwa zikifanyika katika eneo hilo sambamba na kutoa burdani kwa wananchi wake.

Mapema Waziri huyo, alisema mbali na hayo wananchi walishughudia burdani ya mashindano ya Mapinduzi Cup yalioanza Januari 5 na kuzinduliwa na Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleimana Abdalla huku Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Katika hatua nyengine, Dk. Khalid alisema wakati Wazanzibari wanatimiza miaka 57 ya Mapinduzi Zanzibar nchi imepiga hatua ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii jambo ambalo wananchi wanapaswa kujivunia.

Alisema mafanikio hayo yametokana na jitihada kubwa zilizochukuliwa na serikali kwa kuimarika misingi imara ya ushirikiano, umoja, moyo wa uzalendo uliowekwa na mzee Abeid Amani Karume.

“Hivyo wananchi wote hatuna budi kuendelea kuyatunza, kuyalinda, na kusheherekea Mapinduzi hayo kila mwaka”, alisema.