NA MWAJUMA JUMA

SHIRIKA  la Bima la Taifa Tanzania  limetoa shilingi milioni 14.7 ikiwa ni mchango wao katika kufanikisha michuano ya kombe la Mapinduzi yanayoanza leo visiwani Zanzibar.

Fedha hizo walizikabidhi jana kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita huko katika Ofisi yake Migombani mjini Unguja.

 Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Elirehema Doriye, alisema fedha hizo walizotoa zitatumika wa ajili ya mchezaji bora wa kila siku pamoja na shughuli za uendeshaji wa mashindano hayo.

Sambamba na hayo alisema watakuwa washirika wa kusaidia michuano hiyo kwa muda wa miaka mitatu.

Nae Waziri wa Habari, Vijana, Utumaduni Sanaa na Michezo Tabia Maulid Mwita alisema wizara yake itatoa mashirikiano ya moja kwa moja na shirika hilo katika kufanikisha mipango mbali mbali yanayohusu wizara hiyo.

Hivyo alisema kwa kuwa mambo hayo yanaubeba utambulisho wa wazanzibari, hivyo kushirikiana kwao kutawanyanyua zaidi.

“Naamini wizara yetu imebeba vitu vingi na inahitaji kushirikiana na mashirika tofauti likiwemo hili la Bima, kwa hivyo mtakapokuwa na mawazo, program ambazo mnahisi zinatuhusu sisi karibuni sana na milango ipo wazi”, alisema.