Yaitandika FC Platinums maba0 4-0

NA MWANDISHI WETU

WAWAKILISHI wa Tanzania bara katika ligi ya mabingwa Afrika Simba SC, wamefanikiwa kwenda hatua ya makundi ya ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya FC Platinums ya Zimbabwe.

Mchezo huo wa marudiano ulipigwa jana majira ya saa 11:00 jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Simba SC inaingia hatua hiyo kwa ushindi wa jumla wa 4-1 kufuatia kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Jumatano iliyopita mjini Harare.

Hii inakuwa mara ya tatu kwa Wekundu hao wa Msimbazi kutinga hatua ya makundi baada ya mwaka 2003 walipoitoa Zamalek ya Misri waliokuwa mabingwa watetezi na 2018 walipoitoa Nkana FC ya Zambia.

Simba SC inayofundishwa na Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Erasto Edward Nyoni kwa penalti dakika ya 39 baada ya beki mwenzake, Shomari Salum Kapombe kuvutwa jezi na Tawana Chikore.

Kipindi cha pili Kapombe akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 61 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Francis Tizayi kufuatia shuti la kiungo Mzambia Rally Bwalya.
Nahodha John Raphael Bocco aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya mshambuliaji mwenzake, Mnyarwanda Meddie Kagere akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 90 na ushei akimalizia pasi ya Bwalya tena.

Mzambia mwingine, mchezaji bora wa ligi kuu ya Tanzania bara, kiungo Clatous Chotta Chama akaifungia Simba SC bao la nne kwa penalti dakika ya 90 na ushei baada ya yeye mwenyewe kuvutwa kwenye boksi na Gift Bello .

Kagere aliingia dakika ya 76 kuchukua nafasi ya mshambuliaji mwingine, Mkongo Chris Mutshimba Kope Mugalu lakini akaumia dakika ya 85 na nafasi yake ikachukuliwa Bocco.

Droo ya hatua ya makundi ya michuano hiyo itafanyika Ijumaa Saa 8:00 mchana makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mjini Cairo, Misri.