NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Mohammed Said, ameziagiza skuli binafsi zote kuhakikisha zinafuata mitaala na mihutasari rasmi iliyoidhinishwa na serikali.

Waziri huyo alitoa agizo kwenye taarifa maalum aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, ambapo alisema skuli zote za serikali na binafsi, lazima zihakikishe mitaala na mihutasari inakamilishwa kwa wakati.

Simai alisema ili wanafunzi wafaulu vizuri mitihani yao lazima walimu wafundishe kwa kufuata mitaala na mihutasari, ambayo serikali imeiidhinisha na si vyenginevyo.

Aidha kupitia taarifa hiyo, waziri huyo aliwaomba wazazi, walezi, walimu na wadau wengine wa elimu wazidishe mashirikiano katika malezi ya watoto ili jamii iwe na kizazi chenye elimu bora itakayowajengea ufahamu.

Kuhusu suala la ada zinazotozwa kwa skuli binafsi, Simai alisema alizishauri skuli hizo zizingatie hali ya maisha iliyopo kwani skuli zipo kwa lengo la kutoa huduma kwa jamii na kuendelea kuisaidia serikali katika lengo lake la kutoa elimu bora.

Waziri huyo pia alizishauri skuli binafsi ambazo wanafunzi wake wanatarajiwa kufanya mitihani ya taifa ya kidato cha sita mwezi Mei mwaka huu, kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliosajiliwa wanaruhusiwa kufanya mitihani yao bila ya kikwazo.

Kuhusu usafiri wa wanafunzi kwa skuli binafsi, waziri huyo alitoa agizo kwa uongozi wa skuli zinazotumia usafiri wa mabasi kuhakikisha kuwa wanapakia wanafunzi kama idadi inavyoruhusu na madereva kuzingatia usalama barabarani.

“Skuli yoyote ambayo itapakia wanafunzi zaidi ya uwezo wa basi husika taratibu za kisheria zitachukuliwa dhidi ya skuli hiyo. Aidha, tunazitaka skuli zote zinazotumia usafiri wa mabasi kuweka alama ya utambulisho wakati wanapowapakia wanafunzi”, alisema waziri huyo.

Waziri huyo aliwashauri wazazi na walezi kutowapa vyombo vya moto wanafunzi ambao hawajafikia umri wa miaka 18 ili kuepusha madhara yatakayojitokeza na kuziagiza mamlaka zinazosimamia suala la usalama barabarani zichukue hatua zinazostahiki kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Katika taarifa yake hiyo, waziri huyo aliagiza kuwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ufanyike usafi katika maeneo yote ya majengo ya taasisi zinazotoa elimu kuanzia maandalizi hadi vyuo vikuu kwa Unguja na Pemba.

Muhula wa masomo kwa wanafunzi wa Zanzibar kwa mwaka 2021 unatarajiwa kuanza rasmi Januari 18 mwaka huu na utamalizika Disemba 10 mwaka huu, ambapo kutakuwa na jumla ya wiki 43 za masomo.