KWA takriban miaka 57 sasa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza kwa vitendo sera iliyoiasisi baada ya mapinduzi ya mwaka 1964 ya elimu bure.

Serikali inaposema elimu bure maana yake inagharamia huduma za kielimu kwa watoto wa Zanzibar, kwa mfano mishahara na stahiki za walimu, gharama ujenzi wa skuli zenyewe, gharama za kuchapisha mitihani, gharama vifaa nakadhalika.

Kimsingi gharama hizo zote kama zisingebebwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, maana yake ni kwamba kila mzee mwenye mtoto angepaswa kumlipia mtoto ili apate nafasi kupata elimu.

Kwa mwaka huu tayari msimu mpya wa msomo kwa wanafunzi wa skuli za umma na binafsi umeshafunguliwa ambapo kwa mujibu wa taarifa rasmi ya wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wanafunzi watasoma kwa wiki 43.

Aidha katika kalenda ya mwaka huu wa masomo, wanafunzi wa skuli za serikali na binafsi watahudhuria siku 213 za masomo madarasani na watakuwa na wiki saba za mapumziko.

Kama hiyo haitoshi wanafunzi wote wa skuli za serikali na binafsi watasomo mtaala mmoja na mihutasari rasmi iliyoidhinishwa na serikali, kwa hakika huu ni mpango mzuri sana wneye kulenga kuwa na mfumo mmoja wa elimu katika nchi.

Tunaipongeza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu awamu ya kwanza hadi awamu ya nane kwa kuendeleza sera ya elimu bure, kwani kwa hakika tunda hilo la mapinduzi limewanufaisha wengi.

Hata hivyo, kwa kuzingatia mchango wa sekta binafsi katika kukuza maendeleo na utoaji wa huduma za jamii, serikali ya Mapinduzi haikusita kukubali kuanzishwa skuli za binafsi.

Hivi sasa hapa Zanzibar kila kipembe hasa katika miji mikubwa imejaa skuli binafsi, huku nyengine ikiitwa za kimataifa ‘international’, lakini ukiitizama kwa jicho jengine utashangaa kwanini skuli hiyo iitwe ‘international school’.

Lazima tukiri kwa upande mwengine zipo skuli binafsi zinakiwango cha kuitwa ‘international’ sio kwa mandhari tu ya skuli hizo, lakini hata walimu wenye uwezo, wenye kufundisha kwa mipango lakini pia kulipwa vizuri.

Kwa tunavyofahamu serikali imeruhusu na kuridhia kuanzishwa skuli binafsi ili kusaidia utoaji wa huduma za kielimu kwa watoto wa Zanzibar, lakini kinachoshangaza zipo wapo baadhi ya wadau wa elimu wameifanya tasnia ya elimu kuwa biashara.

Tunasema hivyo kwa sababu baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa skuli hizo wanawakomoa wananchi wanaowapeleka watoto wao katika skuli za binafsi, kwa kila mwaka kuongeza bei.

Unaweza kushangaa lakini ukweli ni kwamba kuna baadhi ya skuli hapa Zanzibar mwanafunzi wa skuli ya msingi ada yake ni kubwa kwa mwaka kiasi cha kumkaribia mwanafunzi wa chuo kikuu.

Kwa bahati mbaya sana baadhi ya skuli za binafsi kila mwaka zinaongeza bei, hali hiyo inatokana na kwamba hakuna bodi maalum ambayo itamlinda mzazi anayelipa ada, hivyo ama kulipa ada ama kumtoa mwanawe katika skuli hiyo endapo atashindwa kulipa.

Tunadhani ni vyema sana wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ikaangalia mfumo mzima wa skuli binafsi kwa kuzifanyia ukaguzi kwa sababu nyengine ziko kwenye majengo yasiyotahiki kuitwa skuli, lakini utashangaa zinaitwa ‘international school’.

Lakini pia ni vyema wizara ikawa na bodi ambayo itajumuisha skuli binafsi ili kuangalia bei zinazotozwa kama ada kwa wanafunzi, kwani skuli nyengine mzazi analazimika kujikaba mno.

Tuishie kwa kusema kuwa elimu iwe huduma na tusiigeuze kuwa biashara. Tutekeleze wajibu wetu wa kuijenga nchi yetu kwa kila mmoja kuwajibika.