NA FAT-HIYA MOHAMED
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali yake itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo, ili kuhakikisha malengo ya uchumi wa buluu yanafikiwa.
Akizungumzia kwa niaba yake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohammed Said, wakati wa sherehe za uwekaji jiwe la msingi na ufunguzi wa majengo ya Skuli ya Assalam iliopo Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja, amesema kufikia malengo ya maendeleo kunahitaji kushirikiana na kila mdau wa maendeleo hasa katika sekta ya elimu .
Amesema Serikali ya awamu ya nane itaendelea kuwa karibu na wawekezaji wa maendeleo kwa kuwaelekeza namna ya kufata miongozo mbalimbali bila ya kuvunja sheria ili kufikia malengo.
Said amesema Skuli za kijamii nazo ni miongoni mwa vyanzo vizuri vya maendeleo katika jamii, hivyo Wizara ya elimu itaendelea kuwa pamoja nao kwa kuwapa muongozo ya sera ya elimu ya Zanzibar, ili kwenda sambamba na utoaji wa elimu kwa wote.
Amesema uongozi wa Assalam umefanya jambo zuri kuhakikisha wanawekeza katika sekta ya elimu na ujasiriamali vijijini, kitu ambacho kitawapelekea wanakijiji kujiajiri wenyewe kutokana na ujuzi waliopatiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kusini , Rashid Makame Shamsi, amesema ataendelea kusimamia maendeleo ya Wilaya yake hasa katika sekta ya Elimu, kwani hiyo ni sekta ambayo huzalisha wataalamu wote duniani.
Nao wamiliki wa skuli hiyo, Sadiki Mohammed Ali na Hatice Colak, wamesema lengo la kuanzisha Skuli katika kijiji cha Kizimkazi na vijiji jirani ni kuhakikisha wanatoa elimu ya awali na msingi na wanasaidia wanawake, watoto,wazee pamoja na watu wenye mahitaji maalum.
Wamesema pia wana Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ambayo inajishughulisha na maswali mbalimbali ya kijamii ikiwemo uchimbaji wa visima katika vijiji mbalimbali na kuwasaidia watu walio na hali ngumu kimaisha.
Skuli ya Assalam Community Foundation, imeanzishwa mwaka 2017, ili kutoa taaluma kwa wananchi wa Zanzibar hasa vijijini.