NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imeanza kuchukua jitihada la kulihifadhi jengo la Beit el Ajab ili lisiendelee kuanguka.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Lela Mohammed Mussa aliyasema hayo wakati akizungumza na Zanzibar leo.

Alisema tayari utaratibu wa kuanza kulihifadhi jengo hilo umeshaanza vifaa vyote vinavyohitajika vimeshapatikana.

Aidha alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kumaliza shughuli za uokozi na sasa wameona umuhimu wa kulinusuru jengo hilo kwani linaninginia dari, maguzo yaliyopinda na madhari yake haipo katika hali vizuri.

Aidha alisema jengo hilo linawekewa miega pembeni ili lisiendelee kuanguka na kufunikwa viambaza vyake ili kulihifadhi vizuri katika kipindi hichi cha mvua.

“Tunakwenda kwenye kipindi cha mvua maji ya mvua yakiingia kwenye udongo na chokaa litamumunyuka tena hatutaki kufikia huko,” alisema. 

Waziri Leyla alibainisha kuwa jengo hilo lipo katika hali hatarishi tangu lilipanguka na serikali ilichukua hatua ya kwanza kunusuru maisha ya watu.

“Tunalotaka kwanza ni kulihifadhi alafu baadae tutakaa pamoja na na wenzetu wa serikali ya Oman ili tuone vipi ujenzi utaendelea katika kurudisha hadhi ya jumba letu hili lilobeba historia kubwa ya Zanzibar,” alisema. 

Hata Hivyo Waziri Lela, alibainisha kwamba kitu cha msingi wanachokiangalia zaidi katika kulihifadhi jengo hilo ni usalama wa watu ambao wanafanya kazi hiyo.

Alisema jengo hilo lipo chini ya mkandarasi lakini ameshindwa kazi yake toka lilipopata ajali na wameona serikali walisimamie wenyewe kwa kushirikiana na Balozi wa Oman ambao wamekubali kusaidia pesa za ukarabati wa jengo hilo.

Akizungumzia majeruhi waliolazwa hospitali alisema hali zao zinaendelea vizuri na mmoja ameshapatiwa ruhusa ya kurudi nyumbani.

Waziri Lela alitumia nafasi hiyo kuwaahidi wananchi  wa Zanzibar kuwa serikali itafanya kila jitihada kuona jengo hilo linarudi katika nafasi yake.