ZASPOTI
KIUNGO, Timothy Fosu-Mensah ataruhusiwa kuondoka Manchester United mwezi huu, bosi Ole Gunnar Solskjaer amethibitisha.
Yoso huyo wa Uholanzi alijiunga na United akitokea akademia ya Ajax akiwa na umri wa miaka 16 mwaka 2014.


Alicheza mechi yake ya kwanza miaka miwili baadaye kama mbadala dhidi ya Arsenal mnamo Februari 2016, mchezo ambao ulimshuhudia Marcus Rashford, akifunga mara mbili kwenye mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya England.
Lakini, tofauti na Rashford, Fosu-Mensah ameshindwa kuingia kikosini mara kwa mara, akifanya maonyesho 29 tu zaidi katika kipindi cha miaka mitano.


Wakati huo, Fosu-Mensah ametumia muda kwa mkopo huko Crystal Palace na Fulham, na sasa ataruhusiwa kuondoka Old Trafford moja kwa moja endapo ofa sahihi itaingia.
“Sina hakika ikiwa Timo atabakia au [ikiwa] atachukua chaguo sasa,” Solskjaer aliwaambia waandishi wa habari.


“Hajacheza vya kutosha, kwa hivyo ameruhusiwa kuzungumza na klabu, kwa nia ya kuondoka sasa Januari. Ni ngumu wakati una wachezaji wazuri, wachezaji wenye vipaji, na huwezi kuwapa wakati wa mchezo. Sasa yuko katika hatua ambayo anahitaji kwenda kucheza tena.


“Huenda ikawa [mwishoni] mwa Januari, au inaweza kuwa katika msimu wa joto anapata mahali pengine. Kwa hivyo anafanya kazi kwa bidii, Tim, yuko tayari kuhamia kwenye klabu yoyote ambayo anahisi iko tayari”.


Fosu-Mensah, ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu, huenda atakuwa mmoja wa wachezaji wanaoruhusiwa kuondoka Manchester United mwezi huu wakati Solskjaer anaendelea kukijenga kikosi chake.
Raia huyo wa Norway tayari amethibitisha kuwa Sergio Romero na Marcos Rojo wanaweza kuondoka, iwe Januari au wakati mikataba yao inapomalizika majira ya kiangazi.


Odion Ighalo pia anaweza kuwafuata kupitia mlango wa kutokea. Mkataba wa mkopo wa mshambuliaji huyo unaisha mwishoni mwa mwezi na hautafanywa upya.
Kilichoingia tu hadi sasa ni kuwasili kwa winga kijana, Amad Diallo, ambaye alimwaga wino akitokea Atalanta mapema wiki hii
Mkataba wa yoso huyo mwenye wa miaka 18 unaweza kuwagharimu mashetani wekundu hadi pauni milioni 37.(Goal).