DAMESKI, SYRIA
WIZARA ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imelaani mashambulio ya kigaidi yaliyotokea katika mji mkuu wa Iraq Baghdad na kusisitiza ulazima wa kuweko umoja na mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya kupambana na ugaidi.
Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria ilieleza kuwa, mashambulio haya ya kijinai kwa mara nyengine tena yaliweka wazi ukweli huu kwamba, juhudi za kupambana na ugaidi haziwezi kuzaa matunda madhali ugaidi huo haujaangamizwa kikamilifu na hakujawa na umoja na mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya vita hivyo.
Kadhalika taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria ilibainisha kuwa, ugaidi ungali tishio kwa usalama na uthabiti wa kieneo na ulimwengu kwa ujumla.
Baghdad ilishuhudia miripuko miwili pacha ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na idara ya ulinzi wa raia ya Iraq watu 32 walipoteza maisha na makumi ya wengine kujeruhiwa.
Brigedia Jenerali Hazem al Azzawi Mkurugenzi wa Kamati ya Oparesheni ya Baghdad aliliambia shirika la habari la Iraq (INA) kuwa, miripuko pacha ilitokea katika soko lenye watu wengi katika eneo la Bab al Sharji karibu na maidani ya al Tayran.
Mataifa na viongozi mbalimbali wa dunia sambamba na kutoa mkono wa pole kwa serikali, wananchi na familia za Iraq zilizopoteza ndugu na jamaa zao katika shambulio hilo la kigaidi, walilaani vikali kitendo hicho cha kigaidi.