NA ABOUD MAHMOUD
VIJANA nchini wametakiwa kushirikiana na kusaidiana katika kutatua matatizo mbali mbali yanayowakabili ikiwemo suala la ajira.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita wakati akizindua Jumuiya ya ‘Labor’s Empowerment Organization’ (LEO) katika ukumbi wa hoteli ya Madidat el Bahr iliyoko Mbweni.
Waziri Tabia alisema vijana wana wajibu wa kuhakikisha wanasaidiana kwa kutengeneza ajira ambazo ni za kuajiriwa au kujiajiri wenyewe kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili.
Alisema kwamba inafahamika kuwa vijana ndio wengi wenye kuhitaji ajira ambazo zitakua rasmi au zisizo rasmi tofauti na wazee ambao wameshafika umri wa miaka 60.
“Nakuombeni vijana wenzangu kushirikiana na kusaidiana katika kuliondosha hili tatizo ambalo linawakabili vijana wengi, naamini mashirikiano yenu yataweza kutatua tatizo hili,” alisema.
Tabia alisema wizara yake itachukua jitihada mbali mbali kuhakikisha inaipa jumuiya hiyo mashirikiano ya kutosha kwa lengo la kuwafikia vijana wote nchini Tanzania.
Alisema LEO haina jukumu la kuwasaidia vijana wa Unguja na Pemba peke yake bali jukumu lao ni kuwasaidia vijana wote waliopo nchini Tanzania kutokana na wote ni ndugu waliotokana na ASP na TANU.
Aidha Waziri Tabia alitoa ushauri kwa jumuiya hiyo kupanga mpango wa kupita vijijini hususan katika maeneo ambayo yana vijana wengi wenye uhitaji wa ajira lakini hawajui waanzie wapi.
Alisema wapo vijana ambao hawajui kwamba zipo fursa kutoka Serikalini au kwa taasisi binafsi ambazo zinaweza kuwasaidia kuwapa elimu ya kuwasaidia kuhusiana na tatizo na ajira.
Alifahamisha kwamba faida kubwa itakayopatikana ya kutoa elimu ya ajira mjini na vijijini wataweza kupambana na utumiaji wa dawa za kulevya kwa vijana.
Alisema vijana wengi wamejitumbukiza katika dimwi la utumiaji wa dawa za kulevya kutokana na kukosa ajira na kutojua nini cha kufanya.
Aidha Waziri huyo aliipongeza Jumuiya hiyo ambayo imejipanga kuwasaidia vijana wenzao kwa lengo la kutatua changamoto mbali mballi zinazowakabili.
Akisoma risala ya Jumuiya hiyo, Katibu wa LEO, Fatma Suleiman Sarahan alisema jumuiya yao ni zao kutoka taasisi ya ‘Friends of Mwinyi’ iliyozinduliwa August 22 mwaka jana.
Alisema vijana wa Friends of Mwinyi kwa kutambua fursa ambazo vijana wanaweza kuzipata waliamua kuunda jumuiya hiyo itakayowakutanisha wenye uwezo na ustadi mbali mbali kwa kutumia fursa ya nguvu ya ujana wao katika kujikwamua kiuchumi na kisiasa.
Katika risala ilisema jumuiya yao ina malengo matano ikiwemo kubuni miradi na kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kuunga mkono ajira katika sekta ya elimu, kilimo, afya, utalii na mazingira.
Mengine ni kuhimiza vijana juu ya suala la kujiajiri kama nyenzo za kupigana na ukosefu wa ajira, kuhamasisha na kuwawezesha vijana kwa kuwapa ujuzi wa kuwasaidia katika kutambua na kutumia uwezo wao.
Aidha malengo mengine ya taasisi hiyo ni kufanya shughuli zote husika ikiwemo utekelezaji wa miradi itakayofadhiliwa na Serikali pamoja na nchi za karibu pamoja na kufanya kazi na viongozi wote wa Serikali.