NA MWANDISHI WETU

TANZANIA imeanza vibaya fainali za ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), baada ya kufungwa mabao 2-0 na Zambia katika mchezo wa Kundi D uwanja wa Omnisport Jijini Limbe.

Huo unakuwa mchezo wa sita mfululizo kwa Taifa Stars kucheza bila kushinda tangu ishinde dhidi ya Equatorial Guinea Novemba 15, mwaka 2019 kwenye mechi ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mechi zilizofuata Stars ilichapwa mabao 2-1 na Libya nchini Tunisia kufuzu AFCON, ilichapwa 1-0 na Burundi kirafiki  Dar es Salaam, ikachapwa 1-0 na Tunisia kufuzu AFCON Tunis, ikatoa sare za 1-1 mfululizo nyumbani na Tunisia kufuzu AFCON na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kirafiki uwanja wa Mkapa.

Kwa matokeo hayo, Taifa Stars inayofundishwa na kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije imejiweka njia panda kwenda hatua ya mtoano kwenye mbio za kuwania kombe la michuano inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee. 

Kwa Zambia inayofundishwa na kocha Mserbia, Milutin Sredojevic imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kuingia hatua inayofuata baada ya ushindi huo.

Mshambuliaji wa NAPSA Stars, Collins Sikombe alipewa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi baada ya kufunga bao moja na kusababisha la pili.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, alifunga kwa penalti dakika ya 64 baada ya beki mkongwe wa Tanzania, Shomari Kapombe kuunawa mpira kwenye boksi katika harakati za kuokoa, kabla ya kumpa pasi  mshambuliaji wa Nkwazi FC, Emmanuel Chabula kufunga la pili dakika ya 81.

Taifa Stars itarudi uwanja wa Omnisport Jijini Limbe Jumamosi kumenyana na Namibia kabla ya na kukamilisha mechi zake za Kundi D kwa kucheza na Guinea uwanja wa Reunification, Douala Januari 27.