NA FARIDA MSENGWA, MOROGORO

KITUO cha kitaifa cha kuratibu hewa ukaa kimefanikisha utafiti wa takwimu wa hewa ukaa kwa awamu ya kwanza katika kipindi cha mwaka 2008-2015 kwa ufadhili wa jumuiya ya ulaya EU huku kikijipanga kwa awamu ya pili ya utafiti kwa kipindi cha mwaka 2013, mpaka 2020, ili kuona jinsi gani kuna upotevu wa rasilimali misitu.

Akizungumza na waandishi wa habari walipotembelea kituo hicho kilichopo katika chuo kikuu cha kilimo SUA ,Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha kuratibu hewa ukaa (NCMC) Prof Eliakimu Zahabu, alisema takwimu hizo ni tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016 kikiwa na lengo la kudhibiti hewa ukaa itokanayo  na misitu.

Hata hivyo,  Prof Zahabu, alisema mwaka 2018 waliweza kufanikiwa kuwakilisha takwimu za msingi  kwa kufanya utafit chini ya shirika la chakula  FAO na kushirikiana na TFS ambapo  taarifa zilipelekwa umoja wa mataifa ambapo ilionekana kwamba Tanzania ndiyo nchi pekee iliyofanya utafiti kwa kutumia wataalamu wake.

Alisema katika nchi nne Tanzania ndiyo iliyotumia wataalamu wake wa ndani na kufanikiwa kuwajengea uwezo wataalamu wake wa ndani pamoja na miundombinu ya kuweza kufanikisha  takwimu na hivyo kuongezewa  jukumu jengine la kuchakata takwimu za gesi joto kwenye sekta ya Misitu, kilimo, Nishati Viwanda na Taka.

Prof Zahabu, alisema  mpaka sasa wataalamu wao wameweza kuuchakata takwimu zote pekee bila ya msaada wa wataalamu kutoka nje na kwa sasa wanataka kuziboresha zaidi takwimu toka mwaka 2013  mpaka sasa hivyo mchakato bado unaendelea wa mjadala na FAO, ili kuweza kuwa na takwimu nyingine za miti ili kuweza kupata takwimu zote za misitu nchini.

Aidha alisema sensa ya misitu huwa inatoa taarifa ili kujua aina za misitu iliyopo na imechukua ukubwa gani wa ardhi nchini ambapo ilionekana hekta 48  elfu ndiyo inayopotea ambayo ni zaidi ya eneo la nchi, ambapo walitengeneza ramani yenye kuonesha upotevu wa misitu kwa mwaka na wakapata hekta laki nne na sabini  zinapotea kila mwaka kwa ajili ya upotevu wa misitu hasa kanda ya magharibi  katika mikoa ya kigoma tabora na katavi.

Alisema mikoa hiyo, inaongoza kwa upotevu huo wa ardhi kutokana na tatizo la wakimbizi kwakuwa wanatumia nishati ya kuni,kilimo cha tumbaku ambapo wanatumia nishati ya kuni kwa ajili ya kukaushia tumbaku na kukata misitu kwa ajili ya upanuzi wa mashamba lakini pia wafugaji wengi waliopo kanda ya ziwa wanachangia hasa mikoa ya magharibi.

‘’Ingawa kazi kubwa tunayoifanya ni kuzalisha takwimu lakini linapotokea tatizo kubwa huwa tunaenda eneo husika kwa ajili ya kujadiliana na wadau juu ya tatizo hilo na kulikabishi katika mkoa husikaili walifanyie kazi’’alisema Prof Zahabu.