WASHINGTON, MAREKANI

RAIS anayeondoka wa Marekani Donald Trump amesema vizuizi dhidi ya wasafiri kutoka Ulaya na Brazil vitaondolewa kuanzia Januari 26, ijapokuwa utawala unaoingia madarakani  wa Biden umejibu kuwa vizuizi hivyo vitaendelea kutekelezwa.

Trump, ambaye amebakia saa chache kabla ya kuondoka madarakani, alisema katika tangazo kuwa kuingia bila vizuizi nchini Marekani kwa watu ambao walizuru eneo la Ulaya la Schengen, Uingereza na Brazil hakuna tena madhara kwa maslahi ya Marekani.

Alisema uamuzi huo ulichukuliwa kutokana na ushauri wa kiafya, baada ya Shirika la Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa nchini Marekani CDC kutoa amri kuanzua Januari 26, inayowataka abiria wote wa ndege wanaoingia Marekani kutoa ushahidi wa vipimo vya corona.

Muda mfupi baada ya tangazo hilo, msemaji wa Rais Mteule wa Marekani Joe Biden akasema utawala unaoingia hauna nia ya kuondoa vikwazo vya safari za kimataifa.