NA TATU MAKAME

MAMLAKA ya mapato Tanzania (TRA) upande wa Zanzibar imesema itahakikisha inaongeza kiwango cha ukusanyaji mapato kupitia vyanzo mbali mbali, ili fedha hizo zinatumike kwa maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.

Ofisa Msimamizi wa kodi Abdalla Seif Abdalla, alisema hayo Ofisini kwake Mlandege Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja wakati alipozungumza na Gazeti hili.

Alisema Mamlaka itahakikisha inafuatilia madeni ya kodi kuona kila mfanyabiashara analipa kodi kwa wakati kufikia azma ya Serikali ya kukusanya kodi.

Kauli ya Ofisa huyo imekuja kufuatia mamlaka hiyo kukusanya shilingi bilioni 68.7 sawa na asilimia 72.6 kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2020.

Hata hivyo, alisema mamlaka hiyo ilikusudia kukusanya shilingi bilioni 94.6 kwa kipindi hicho, lakini kiwango hicho hakikufikiwa kutokana na kupungua kwa mzunguuko wa biashara.

Alibainisha kwamba mamlaka itafanya kila jitihada kuwahimiza wafanyabiahara kulipa kodi kwa kuendelea kutoa elimu juu ya ulipaji kodi kwa hiari kwa wafanyabiashara.

Alisema njia nyengine itakayotumika kutumia mfumo mpya wa mtandao baada ya kuwasajili wafanyabiashara na wafanyakazi kwa kutumia mfumo wa (tin) kwa njia ya mtandao. Alifahamisha kuwa mamlaka pia itaendelea na ukaguzi wa kodi kwa makampuni mbalimbali na taasisi za serikali kuona kila wafanyabiashara wanalipa kodi kwa wakati.

Hata hivyo, aliwataka wafanyabiashara wenye madeni kwenda kulipa kodi na pia wanaweza kuingia kwenye makubaliano kwa kulipia kwa awamu hadi kumaliza madeni yao.

Aidha aliwasisitiza wafanyabiashara kuendelea kutoa risiti na wateja kudai risiti kila wanapofanya mauzo au kununua bidhaa.

Akizungumzia mfumo wa usajili kwa wafanyakazi wa taasisi mbalimbali za binafsi na serikali pamoja na wafanyabiashara kwa kutumia mfumo wa tin Ofisa huyo alisema zoezi linaendelea vizuri na mwamko umeongezeka.